IQNA

Taarifa ya Harakati ya Kiislamu Nigeria

Serikali ya Nigeria inapanga kumuua Sheikh Zakzaky

12:25 - February 08, 2019
Habari ID: 3471833
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la Nigeria linapanga njama ya kumua kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN), Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa katika kizuizi cha kijeshi.

Katika taarifa siku ya Jumatano, IMN imesema mashirika ya  usalama nchini humo yanapanga kutekeza njama ya kumuua Sheikh Zakzaki kupitia oparesheni bandia ya ufaytulianaji risasi.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema hatua ya serikali kudai kuwa wafuasi wa harakati hiyo wanapanga kutekeleza hujuma dhidi ya magereza wakati wa uchaguzi wa mwezi huu ni sehemu ya njama hiyo. IMN inasema wanajeshi watakaovalia nguo za raia wanalenga kushambulia magereza kadhaa ikiwa ni pamoja na eneo anamoshikiliwa Sheikh Zakzaky na kisha idaiwe kuwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia waliotekeleza hujuma hiyo ili kumuokoa Sheikh Zakzaky. Kwa mujibu wa njama iliyofichuka, katika oparesheni hiyo bandia, ufyatulianaji risasi utajiri na hapo Sheikh Zakzaky atauawa kisha vyombo vya usalama vidai kuwa aliuawa wakati maafisa usalama walipokuwa wakijaribu kuwazuia wafuasi wake waliokuwa wanataka kumtorosha jela. INM imesisitiza kuwa haitumii silaha na inafungamana na sheria za nchi na itafuatilia mkondo wa sheria katika kufuatilia matakwa ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi pamoja na kuwa mahakama imetoa aamri ya kutaka waachiliwe huru.

Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo.

3467880

captcha