IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuiunga mkono Syria ni sawa na kuunga mkono muqawama na tunajifakharisha kwa hilo

14:05 - February 26, 2019
Habari ID: 3471853
TEHRAN (IQNA) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wakati alipoonana na kuzungumza na Rais Bashar al Assad wa Syria hapa mjini Tehran Jumatatu kwamba, Iran inalihesabu suala la kuiunga mkono Syria kuwa ni sawa na kuunga mkono muqawama (mapambano ya Kiislamu) na inaona fakhari kwa jambo hilo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei vile vile amesema kuwa, siri ya ushindi uliopatikana Syria na kushindwa Marekani na vibaraka wake wa eneo hili ni istiqama na kusimama imara rais na wananchi wa Syria na kushikamana kwao na muqawama. Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakuhesabu kuisaidia serikali na wananchi wa Syria kuwa ni sawa na kuisaidia kambi ya muqawama na inajivunia jambo hilo kwa dhati ya moyo wake.

Ayatullah Khamenei amegusia jinsi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyosimama kiukweli pamoja na taifa na serikali ya Syria tangu mwanzoni kabisa mwa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu na kuongeza kuwa, Kutokana na kusimama kwake imara na kwa ushirikiano mzuri wa wananchi, Syria imeweza kukabiliana vilivyo na muungano mkubwa ulioundwa Marekani, Ulaya na vibaraka wao wa eneo hili na imevuka na ushindi katika kipindi hiki kigumu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema kuwa, ushindi wa kambi ya muqawama huko Syria umewahamakisha Wamarekani na ndio maana hivi sasa wanapanga njama nyingine dhidi ya Syria na njama hizo ni hatari sana hivyo kuna wajibu wa kukabiliana nazo vilivyo na kwa nguvu zote. Amesema, miongoni mwa njama hizo hatari ni Marekani kujaribu kujiimarisha katika mpaka wa Syria na Iraq, lakini amesisitiza kuwa maadui watashindwa pia katika njama zao hizo.

Kwa upande wake, Rais Bashar al Assad amesema kuwa, vita vya Syria vinafanana na vita vya miaka minane ilivyolazimishwa Iran kupigana baada ya kuvamiwa na utawala wa wakati huo wa Iraq na kuongeza kuwa, Syria ilikuwa bega kwa bega na Jamhuri ya Kiislamu katika vita hivyo ambavyo taifa la Iran lilipambana kishujaa na kujitoa muhanga kikamilifu kujihami.

Rais Rouhani akutana na Rais Assad

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mipango itakayoainishwa na serikali ya Syria katika kuijenga upya nchi hiyo ya Kiarabu.Kuiunga mkono Syria ni sawa na kuunga mkono muqawama na tunajifakharisha kwa hilo

Rais Rouhani aliyasema hayo katika mazungumzo yake na na Rais Bashar al Assad wa Syria hapa mjini Tehran jana Jumatatu na kuongeza kuwa, serikali ya Iran kama ilivyokuwa huko nyuma, itaendelea kuisaidia na kushirikiana na Syria katika juhudi zake za kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo iliyoshuhudia vita na uharibifu mkubwa kwa miaka kadhaa sasa.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari wakati wote kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na Syria katika kiwango cha kiistratijia na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Damascus katika nyuga mbalimbali.

Amesema ushirikiano wa pande kadhaa wa nchi za Mashariki ya Kati umechangia pakubwa katika kurejesha usalama na uthabiti katika eneo hili.

Kwa upande wake, Rais Bashar al Assad amesema kuwa, serikali na taifa la Syria kwa ujumla linaishukuru Iran kwa kuwaunga mkono Wasyria hususan katika vita dhidi ya ugaidi. Hali kadhalika ameipongeza serikali ya Tehran kwa jitihada zake za kurejesha amani na utulivu sio tu nchini Syria bali katika eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla.

3793357

captcha