IQNA

20:59 - March 08, 2019
News ID: 3471867
TEHRAN (IQNA)-Wananchi wa matabaka mbali mbali huko Algeria wameendeleza maandamani Ijumaa wakimtaka Rais Abdelaziz Bouteflika aondoke madarakani na asiwanie tena urais mwezi ujao wa Aprili.

Kwa wiki kadhaa sasa miji mbali mbali ya Algeria imekuwa medani ya wananchi wenye hasira ambao wanataka mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini humo hasa kuondoka madarakani Bouteflika na kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Ijumaa hii makumu ya maelfu ya raia wameandamana dhidi ya Bouteflika katika miji mbali mbali ya Algeria ambapo maandamano makubwa zaidi yameripotiwa katika mji mkuu, Algiers.

Pamoja na hayo, Bouteflika ametoa onyo lake la kwanza kwa maelfu ya raia wanaoandamana kote katika nchi hiyo wakitaka ahitimishe utawala wake wa miaka 20. Amesema kuwa ghasia na machafuko yatayumbisha nchi. Waalgeria wanapinga vikali hatua ya Rais Bouteflika wa nchi hiyo ya kugombea tena kiti cha urais. Bouteflika mwenye miaka 82 na ambaye ni mgonjwa hajawahi kutoka hadharani na kuzungumza tangu apatwe na maradhi ya kiharusi mwaka 2013 na sasa inaelezwa kuwa Rais huyo amelazwa hospitalini mjini Geneva Uswisi. 

Rais wa Algeria tayari amekabidhi fomu zake za ugombea wa kiti cha urais licha ya kusumbuliwa na maradhi. Jumuiya ya Taifa ya Mawakili ya Algeria imeitaka Tume ya Uchaguzi ya Nchi hiyo iakhirishe uchaguzi ujao wa rais na badala yake iunde serikali ya mpito.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Aprili 18, Algeria itapitia kipindi kigumu ambacho kitaainisha mustakabali wa nchi hiyo na kuna uwezekano wa kushadidi machafuko ya kijamii na kisiasa nchini humo.

3468079

Name:
Email:
* Comment: