IQNA

Magaidi waua watu zaidi ya 207 katika hujuma Sri Lanka

19:37 - April 21, 2019
Habari ID: 3471923
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wameua watu wasiopungua 207 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 500 katika wimbi kubwa la hujuma ambazo zimelenga makanisa na mahoteli nchini Sri Lanka .

Taarifa zinasema milipuko minane ya mabomu imelenga maeneo tafauti huku ikionekana kuwalenga waumini waliokuwa wakishiriki katika ibada za Pasaka makanisani.

Makanisa yaliyolengwa katika hujuma hizo za kigaidi ni pamoja na  Kanisa la St. Anthony Church mjini Colombo Kanisa la St. Sebastian katika mji wa karibu wa Negombo na pia Kanisa la Zion katika mji wa mashariki wa Batticaloa.

Magaidi pia wamelenga hoteli nne za kifahari na nyumba binafsi mjini Colombo. Hoteli ya kifahari ya Cinnamon Grand kati kati ya mji wa Colombo ambayo hutumiwa sana na wanasiasa pia imelengwa katika hujuma hiyo. Hoteli zingine zilizolengwa ni Shangri-La na Kingsbury.

Waziri wa Ulinzi  wa Sri Lanka Ruwan Wijewarden amesema uchunguzi umebaini kuwa magaidi waliokuwa wamesheni mabomu ndio waliotekeleza mashabulizi hayo ya leo asubui na kwamba wote walikuwa wanachama wa kundi moja. Aidha amesema raia 27 wa kigeni ni miongoni mwa waliouawa.

Rais Maithripala Sirisena amesema ameamuru kikosi maalum cha polisi na jeshi kuchunguza aliyehusika na mashambulizi hayo pamoja na kiini chake. Msemaji wa jeshi amesema askari wametumwa kuweka ulinzi na usalama umeimarishwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Colombo.

Kufuatia hujuma hiyo, wakuu wa Sri Lanka wametaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liitishe kikao cha dharura.

Hakuna kundi ambalo limedai rasmi kuhusika na mashambulizi hayo katika nchi ambayo ilikuwa vitani kwa miongo mingi na wapiganaji waliotaka kujitenga wa Tamil Tigers hadi mwaka wa 2009.

Wakati huo huo Waislamu nchini Sri Lanka wamejitokeza kulaania hujuma hizo za kigaidi katika Jumapili ya Pasaka nchini humo.

Baraza la Waislamu nchini Sri Lanka limetoa taarifa likisema linaomboleza mauaji ya watu wasio na hatia ambayo yametekelezwa na watu wenye misimamo ya kufurutu adha wanaolenga kuibua hitilafu za kidini na kikamu. 

Nalo Barazal la Maulama nchini humo ambalo linajulikana The All Ceylon Jammiyyathul Ulama limesema kuwalenga Wakristo katika maeneo yao ya ibada ni jambo lisilokubalika.

Waislamu ni karibu asilimia 10% ya watu milioni 23 nchini Sri Lanka.

 

3805348

captcha