IQNA

Kiongozi Muadhamu atoa wito kwa taifa la Iran lishikamane katika kukabiliana na njama za adui

12:44 - May 02, 2019
Habari ID: 3471938
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema leo Jumatano wakati huu wa kukaribia maadhimisho ya Siku ya Mwalimu nchini Iran kwamba kama taifa litashikamana na kuwa kitu kimoja, basi njama zote za adui zitamrudia mwenyewe.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo mbele ya maelfu ya walimu waliomtembelea ofisini kwake hapa Tehran na kuzungumzia pia jinsi adui anavyojiandaa kwa vita na mashambulizi yake ya kiuchumi na kisiasa na kujpenyeza kijasusi na kujaribu kushambulia kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Ameongeza kuwa, Marekani na Uzayuni unafanya njama za kila upande dhidi ya taifa la Iran, ingawa suala hilo halimalizikii tu kwa serikali ya hivi sasa ya Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kwa vile adui anajipanga kwa vita dhidi ya taifa la Iran, taifa hili la Kiislamu nalo linapaswa kujipanga kwa vita, hivyo viongozi wote, wananchi wa matabaka yote na watu wenye uwezo na muhimu katika kila uwanja, wana wajibu wa kutambua kuwa wana jukumu la kujiandaa vilivyo na kujiweka tayari katika medani hiyo.

Amesema, inavyoonekana kijuu juu ni kwamba adui hivi sasa hajiandai kwa ajili ya vita vya kijeshi, lakini ni jambo lililo wazi kwamba majeshi na vikosi vyetu vya ulinzi viko macho na havighafilishwi na kitu chochote.

Ayatullah Khamenei amegusia pia hati maarufu ya masomo ya 2030 na sababu inayozifanya nchi za kibeberu kung'ang'ani mno hati hiyo na kufichua uhakika wake akisema: Uhakika wa hati ya 2030 ni kwamba mfumo wa masomo upangwe kwa namna ambayo utatupa nje na kudharau kabisa masomo ya falsafa na utaratibu wa kuishi maisha ya chini na ya kawaida na badala yake mfumo huo ujengwe juu ya misingi ya madola ya Magharibi kwa ajili ya kusomeshwa watoto wadogo na mabarobaro.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepandisha juu bendera ya dini kote ulimwengu na kwamba katika upande wa elimu, Iran hivi sasa ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa za kielimu duniani.

3468419

captcha