IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mfumo wa kibeberu unategemea mabavu ya kisiasa

6:51 - March 31, 2016
Habari ID: 3470221
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, mfumo wa kibeberu uliosimama juu ya msingi wa kutumia mabavu ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijeshi.

Ameendelea kusema kuwa mfumo wa kibeberi haudharau hata fursa moja unayoipata kwa ajili ya kulidhuru taifa la Iran, na inapasa kuwa macho wakati wote kuhusu uhakika huo.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Bibi Fatima Zahra AS mbele ya wasoma kasida za Ahlul Bayt AS na kusema kuwa, mabeberu wanategemea sana uwezo wao wa kijeshi kwa ajili ya kulifanyia ubeberu taifa la Iran.

Ameongeza kuwa, iwapo katika mazingira haya ya sheria za msituni zinazotawala duniani leo; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatosheka tu na kufanya mazungumzo na kuwa na mabadilishano ya kibiashara na hata ya kielimu na kiteknolojia na kusahau kujiimarisha kijeshi, bila ya shaka yoyote suala hilo litakuwa na madhara makubwa kwake, kwani hata nchi ndogo kabisa duniani zitapata uthubutu wa kutoa vitisho kwa taifa la Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewalaumu vikali watu ambao wanaona kuwa mustakbali wa taifa la Iran unaishia tu kwenye mazungumzo na si makombora na kusema kuwa, kama wanaotoa matamshi hayo wanayatoa kwa kujua, basi watambue kuwa huo ni usaliti.

Amesema, mustakbali wa taifa la Iran unategemea mambo yote, vinginevyo, haki ya taifa la Iran itapotea kirahisi sana.

Vile vile amegusia namna maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wanavyotumia nyenzo zao zote - za zamani na za kisasa - katika kuifanyia uadui Iran na kusisitiza kuwa, maadui wanatumia mbinu zote, wanatumia mazungumzo, mabadilishano ya kibiashara, vikwazo, vitisho vya kijeshi na kila wenzo wanaoupata ili kufanikisha malengo yao, hivyo taifa la Iran nalo linapaswa kujiimarisha vizuri katika nyuga zote ili liweze kujihami na kukabiliana vilivyo na njama hizo za maadui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, majaribio ya makomboa yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH hivi karibuni yameyafurahisha mataifa ambayo yanateswa na kunyanyaswa na Marekani na utawala wa Kizayuni na hayawezi kufanya lolote kukabiliana na mbeberu hao.

Aidha amewataka wasoma kasida za Ahlul Bayt AS watumie vizuri vipaji vyao kukabiliana na njama za maadui za kudhoofisha imani za Waislamu na kusisitiza kuwa, inabidi zitumike binu zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiulinzi kwa ajili ya kutia nguvu nafasi ya Iran duniani.

captcha