IQNA

Hatari ya kuibuka vita vikubwa baina ya India na Pakistan

12:57 - February 28, 2019
Habari ID: 3471856
TEHRAN (IQNA) – Katika kipindi cha siku kadhaa sasa kumeibuka uhasama mkubwa baina ya India na Pakistan na kuna hatari ya kuibuka vita kamili baina ya madola hayo mawili yenye makombora ya nyuklia.

Uhasama huo ulianza baada ya India kudai kuwa Shirika la Ujasusi la Jeshi la Pakistan limehusika katika hujuma iliyolenga msafara wa askari usalama wa nchi hiyo mnano Februari 14 ambayo iliua zaidi ya askari 44 wa India katika eneo la Kashmir linalozozaniwa na nchi mbili. Pakistan ilikanusha vikali tuhuma hizo na kusema iko tayari kuisaidia India kufanya uchunguzi.

Lakini pamoja na hayo ndege za kivita za India wiki hii zimeingia katika anga ya Pakistan na kushambulia  ngome za wanachama wa makundi mawili ya kigaidi yanayojiita Jaish-e-Mohammed na Lashgari Tayebeh, kaskazini magharibi mwa Pakistan na kudaia kuwa magaidi 300 wameuawa katika hujuma hiyo. Shambulizi hilo la makombora limejiri katika hali ambayo jeshi la anga la Pakistan limetungua ndege mbili za kivita za India ambazo zilikuwa zimeingia katika anga ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa habari hiyo, ndege moja iliangukia katika ardhi ya Pakistan, huku nyingine ikiangukia katika eneo la India. Kufuatia hatua hiyo nalo jeshi la India limetungua ndege moja ya kivita ya Pakistan aina ya F 16. Viongozi wa India wamesema kuwa leo asubuhi ndege za kivita za Pakistan zilikiuka uhuru wa kujitawala nchi hiyo na kuingia katika anga ya Jammu na Kashmir hivyo jeshi la India lililazimika kujibu na kufanikiwa kutungua ndege moja.

Hadi sasa India na Pakistan zimewahi kuingia vitani mara mbili kuhusu mvutano wa umiliki wa Kashmir na mwaka 1999 pia  kulitokea vita vya moja kwa moja baina ya India na Pakistan katika miinuko la Kargil.

Hata hivyo katika mazingira ya hivi sasa kutokea vita baina ya India na Pakistan hasa kwa kuzingatia uwepo wa tishio la silaha za nyuklia kati ya nchi hizo kunaweza kufuatiwa na hasara kubwa na zisizofidika. 

Kadhia ya Kashmir ni mzozo mkongwe katika historia ya uhusiano wa India na Pakistan, na machafuko ya miongo kadhaa katika eneo hilo yanaonyesha kutokuweko irada ya lazima kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mzozo huo. Kiasi kwamba, katika kipindi cha miaka yote hii, hakujakuweko na uungaji mkono wa kutosha wa nchi zote mbili katika uwanja huu.

Mzozo wa sasa wa New Delhi na Islamabad una tofauti ikilinganishwa na vita vya huko nyuma baina ya pande mbili hizi. Huko nyuma hitilafu zilikuwa ni za moja kwa moja kuhusiana na umiliki wa jimbo la Kashmir, lakini hivi sasa mvutano baina ya India na Pakistan umeathiriwa na harakati za makundi ya kigaidi ambayo serikali ya New Delhi inaituhumu Islamabad kwamba, imekuwa ikiyaunga mkono katika ardhi yake.

Kwa kuzingatia himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa misimamo ya India kwa ajili ya kufanya mashambulio ya ulipizaji kisasi katika ardhi ya Pakistan, kuna uwezekano wa kushadidi mzozo na mvutano baina ya nchi mbili hizo. 

3468019

captcha