IQNA

Mamilioni ya Wairani wajitokeza katika Siku ya Quds kuunga mkono ukombozi wa Palestina

22:33 - May 31, 2019
Habari ID: 3471978
TEHRAN (IQNA) – Mamillioni ya wananchi wa Iran walioshiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo wametangaza azma yao ya kuendelea kuunga mkono ukombozi wa Palestina.

Katika taarifa ya mwisho baada ya maandamano hayo, wamesisitiza kuwa lengo la ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa ni ukombozi wa Quds Tukufu, kukombolewa taifa madhlumu na lisilo na ulinzi la Palestina kutoka katika makucha ya Wazayuni maghasibu na jitihada za kuondoa utawala wa Kizayuni wa Israel katika ramani.



Washiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran katika taarifa yao hiyo wamesisitiza kuhusu kuendelea kuunga mkono harakati ya muqawama, na kukabiliana na mpango hatari ya rais wa Marekani dhidi ya nchi za Kiislamu.

Halikadhalika washiriki wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds wamelaani njama ya Marekani inayojulikana kama 'Muamala wa Karne' na pia hatua ya baadhi ya tawala za Kiarabu katika eneo kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu na bandia wa Kizayuni. Aidha wamelaani kikao ambacho Wazayuni-Wamarekani wamekiandaa huko Bahrain ambacho kinadaiwa kwa ni cha kiuchumi lakini ambacho kinalenga kutekeleza 'Muamala wa Karne' kwa madhara ya Wapalestina na kwa maslahi ya Wazayuni.

Taarifa hiyo imetangaza pia kuunga mkono maandamano ya 'Haki ya Kurejea Wakimbizi Wapalestina' ambayo hufanyika kila Ijumaa na kusema: "Kimya cha taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu kuhusu mauuaji ya umati na jinai zinazotekelezwa na Israel huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi sambamba na kuharibiwa utambulisho wa historia ya Palestina ni mambo ambayo yamewakasirisha Waislam duniani.

Washiriki wa maandamano ya Siku ya Quds mjini Tehran pia wamesisitiza kuwa, njia ya utatuzi wa kadhia ya Palestina ni kuendelea Intifadha, muqawama na mapambano mbele ya waistikbari wa kimataifa, kupinga kusalimu amri na pia kupinga kuwa uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, kuondolewa Israel katika ramani, kurejea wakimbizi Wapalestina na kufanyika kura huru ya maoni yenye kuwajumuisha wote ili kudhamini mustakabali wa Palestina.

Sehemu ya mwisho ya taarifa hiyo imesema: "Marekani ni adui nambari moja wa ubinadamu' sambamba na kulaani hatua ya Marekani kuvunja ahadi na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kuiwekea Iran vikwazo vya kidhalimu na kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

3815976

captcha