IQNA

Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Harakati ya Kiislamu Nigeria

13:57 - September 03, 2019
Habari ID: 3472112
TEHRAN (IQNA)- Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesghulikia masuala ya hukumu zisizofuata sheria na pia mauaji ya kiholela, Agnes Callamard, ameilaani serikali ya Nigeria kwa kutekeleza mauaji na kutumia nguvu ziada dhidi ya Harakati ya Kiislamu nchini humo.

Callamard amesema kuwa matatizo ya kiusalama ya Nigeria yametengeneza mgogoro ambao unahitajia kupewa mazingatio haraka iwezekanavyo, la sivyo utasababisha ukosefu wa usalama katika nchi nyingine za Kiafrika.

Mtaalamu huyo wa haki za binadamu  wa Umoja wa Mataifa aidha amesema kuwa Nigeria imekuwa kama chungu za migogoro ya ndani na kwamba hali inayotawala nchini humo inatia wasiwasi mkubwa.

Callamard ambaye amekuwa katika safari ya kikazi ya siku 12 nchini Nigeria amesema kuwa, polisi na jeshi la Nigeria linatumia nguvu na mabavu kupita kiasi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika vinavyoambata kutofanyika uchunguzi wa kutosha na uwajibikaji.

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kunyonga watu bila ya kufikishwa mahakamani, amesisitiza kuwa, Nigeria inahitajia marekebisho katika taasisi za mahakama, polisi na jeshi ili kukomesha mwenendo wa wananchi kutumia mabavu kutokana na kutopata haki na uadilifu.

Callamard pia amekosoa alichosema ni kunyimwa maisha kwa mabavu na utumiaji wa nguvu kupita kiasi dhidi ya mikusanyiko ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN). Amesema hatua ya kupigwa marufuku harakati hiyo ya Kiislamu inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky ilitegemea dhana tu na kwamba hajapewa ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa kundi hilo lina silaha au ni hatari kwa Nigeria.  

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.

Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo.

3469315

captcha