IQNA

Idadi kubwa ya Waislamu wachaguliwa bungeni Canada

10:42 - October 24, 2019
Habari ID: 3472185
TEHRAN (IQNA) – Katika tukio la aina yake katika historia ya jamii ya Waislamu nchini Canada, idadi kubwa ya Waislamu wamechaguliwa bungeni katika uchaguzi uliofanyika Jumatatu.

Waislamu 11, wakiwemo wanawake wanne, wameshinda viti katika uchaguzi, jambo ambalo linatazamiwa kuleta mabadiliko katika siasa za Canada.

Chama cha Waliberali cha Waziri Mkuu Justin Trudeau kimepata ushindi wa viti 157 ingawa kilihitaji viti 170 ili kuunda serikal moja kwa moja.

Chama cha Wahafidhina kilipata viti 121 na hivyo kushika nafasi ya pili huku chama cha Bloc Quebecois kikipata viti 32 na New Democrats kimepata viti 24.

Wabunge Waislamu waliochaguliwa Canada ni pamoja na Omar Alhabra, Igra Khalid, Ziad Aboulatif, Salma Zahid, Ali Ehsassi, Ahmed Hussein, Majid Jowhari, Maryam Monsef, Yasmin Ratansi, Arif Virani, na Samir Zuberi. Aghalabu ya Waislamu walioingia bungeni ni wa chama cha waziri mkuu Trudeau.

Uislamu ni dini inayoenea kwa kasi zaidi Canada ambapo Waislamu wameongezeka kwa asilimia 82 katika kipindi cha muoongo moja uliopita. Hivi sasa Waislamu ni asilimia 3.2 ya watu wote milioni 35 nchini Canada.

Waisalmu wamepewa nafasi katika serikali ya Canada na kwa mfano hivi sasa Waziri wa Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia ni Ahmed Hussein ambaye ana asili ya Somalia.

Disemba mwaka 2017, Trudeau katika ujumbe wake kwa Kongamano la Kuhuisha Uislamu alisema Waislamu nchini Canada wamekuwa na mchango mkubwa na ni rasilimali muhimu kwa nchi.

"Canada ina bahati kuwa na jamii ya Waislamu wenye harakati," alisema Trudeau katika ujumbe wake maalumu kwa njia ya video.

"Kwa muda wa miaka mingi, Waislamu nchini Canada wameweza kupata ustawi na kutoa mchango mkubwa kwa jamii  huku wakiwa wanadumisha ufungamano muhimu na nchi zao za asili na jambo hilo limewawezesha kuwa na turathi nzuri ya utamaduni."

3852005

Kishikizo: waislamu canada iqna
captcha