IQNA

Vizingiti vikuu katika kufikia Umoja wa Kiislamu kwa mtazamo wa Ayatullah Taskhiri

12:29 - November 14, 2019
Habari ID: 3472214
TEHRAN (IQNA) – Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesisitiza kuwa, kusimama kidete mbele ya njama za kibeberu za maadui wa Umma wa Kiislamu kunahitaji utekelezaji wa mafundisho ya Qurani Tukufu.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri ameongeza kuwa: "Baadhi ya Maulamaa na wasomi ni vizingiti katika kufikia umoja wa Waislamu."
Ayatullah Sheikh Mohammad Ali Taskhiri, alizaliwa Oktoba 19, 1944 katika mji wa Najaf Iraq ni mwanazuoni maarufu wa Kishia nchini Iran. Yeye ni mwanafikra, mfasiri, mwandishi na mtafiti maarufu Muirani na pia amekuwa mstari wa mbele katika kueneza fikra ya umoja wa Kiislamu duniani. Aliwahi kuwa mwakilishi wa mji wa Tehran katika Awamu ya Tano ya Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hivi sasa yeye ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na pia ni mshauri mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya ulimwengu wa Kiislamu. Aidha aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na mwakilishi wa mkoa wa Gilan katika Awamu ya Pili ya Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na Maulid ya Mtume Muhammad SAW, mwandishi wa IQNA, amefika katika ofisi yake mjini Tehran ili kupata kufahamu zaidi kuhusu nafasi ya Al Azhar katika kukurubisha madhehebu za Kiislamu na pia kuhusu vizingiti katika umoja wa Waislamu.
Hii hapa sehemu ya mahojiano hayo.
IQNA: Ni nini mtazamo wako kuhusu Chuo Kikuu cha Al Azhar (cha Misri) na harakati za kukurubisha madhehebu katika chuo hicho?
Ayatullah Taskhiri: Chuo cha Al Azhar kilianzishwa kwa lengo la kukurubisha madhehebu za Kiislamu. Hii ndio sababu iliyopelekea Fatimiyun wa Misri kuanzisha kituo hicho ambacho kinafunza madhehebu tano za Kiislamu (Shia, Shafii, Hanafi, Maliki na Hanbali). Hadi mwaka 1940 Miladia, Al Azhar ilikuwa mbeba bendera ya kukurubisha madhehebu za Kiislamu na iliweza kufanikiwa katika uga huo. Maulamaa wa Al Azhar kwa kushirikiana na Maulamaa wa Qum (nchini Iran) waliweza kuunda Darul Taqrib Bainal Madhahib na taasisi hiyo iliweza kuchukua hatua nzuri katika uga wa kukurubisha madhehebu. Jarida la "Risalatul Islam" na kufunzwa fiqhi ya Imami (Kishia) katika Al Azhar ni kati ya matokeo mazuri ya kuanzishwa Darul Taqrib.
IQNA: Hebu tufahamishe kuhusu hatima ya Darul Taqrib ya Al Azhar.
Ayatullah Taskhiri: Kuanzia mwaka 1940 hadi mwanzoni mwa 1970 Miladia na baada ya kufariki Maulamaa wakubwa wa Al Azhar (nchini Misri) na pia Maulamaa wakubwa wa Kishia katika miji ya Najaf na Qum, harakati za Darul Taqrib zilididimia. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (mwaka 1979) na baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa (vya Iraq dhidi ya Iran kuanzia mwaka 1980 hadi 1988), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kuhusu kuhuishwa Darul Taqrib ya Madhehebu za Kiislamu na hivyo badala ya Darul Taqrib kulianzisha Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ikiwa inafuatilia malengo ya Darul Taqrib iliyokuwa Cairo. Kabla ya kuanzisha jumuiya hii, awali tulijitahidi kuhuhusia Darul Taqrib iliyokuwa Cairo lakini hatukufanikiwa.
IQNA: Kwa mtazamo wako ni vizingiti vipi vikubwa zaidi ambavyo huzuia kupatikana umoja wa Waislamu katika zama hizi?
Ayatullah Taskhiri: Kuna mengi ya kusema katika uga huu; lakini kwa kifupi naweza kusema kuwa, kizingiti kikubwa zaidi katika kukurubisha madhehebu za Kiislamu ni taasubi. Hapa, taasubi ya baadhi ya Maulmaa na wasomi imepelekea baadhi kuwaita wengine kuwa ni makafiri na mafasiki na kuwatuhumu kuwa wameanzisha bidaa.
Kizuizi kingine katika kukuribisha madhehebu za Kiislamu ni ujahili au ujinga. Ukuruba wa madhehebu unakosekana kutokana na ujahili wa baadhi ya Waislamu kuhusu madhehebu za Waislamu wenzao. Iwapo Waislamu watajumuika pamoja na kuelewana basi watafahamu kuwa nukta zao za pamoja ni asilimia 90. Ujahili umeacha athari zake na ndio sababu Waislamu wanatuhumiana na nukta hii ni kizingiti katika umoja. Sababu nyingine inayozuia umoja wa Waislamu ni maslahi binafsi ya tawala ambazo zinashikilia madaraka katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kuna watawala ambao wanaamini kuwa umoja wa Waislamu ni kinyume cha maslahi yao. Aidha ukuruba wa madhehebu za Kiislamu na umoja wa Waislamu ni kinyume cha maslahi ya mabeberu wa dunia na maadui wa Uislamu na kwa msingi huo wanafanya kila wawezalo kuzuia maelewano baina ya Waislamu. Wanaibua mifarakano ya kimadhehebu, kisiasa na kijiografia ili kufikia malengo yao ya kibeberu.

3856095

captcha