IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuondolewa Israel maana yake ni wamiliki wa asili wa Palestina kuweza kuchagua serikali

18:45 - November 15, 2019
Habari ID: 3472216
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuondolewa Israel kuna maana ya kuondolewa utawala bandia wa Kizayuni na mahala pake kuchukuliwa na serikali iliyochaguliwa na wamiliki wa asili wa Palestina ambao ni Waislamu, Wakristo na Mayahudi.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran wakati alipokutana na maafisa wa ngazi za juu katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, washiriki wa Kongamano la 33 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu na watu wa matabaka mbali mbali. Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa: "Maadui wa Uislamu, kinara wao akiwa na Marekani, wanapinga asili ya Uislamu na nchi zote za Kiislamu na silaha yao kuu katika eneo ni 'kujipenyeza katika maeneo hasasi ya uchukuaji maamuzi', 'kuibua mifarakano katika mataifa', na 'kufanya iaminike kuwa kusalimu amri mbele ya Marekani ndio njia ya kutatua matatizo'. Kiongozi Muadhamu amesema mbinu ya kukabiliana na njama hizo ni uelimishaji na kusimama kidete katika njia ya haki.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja daraja za umoja na kusema, daraja ya chini kabisa ambayo ni hatua ya kwanza katika umoja wa Kiislamu ni 'kujiepusha kushambuliana jamii, serikali, kaumu na madhehebu za Kiislamu', na 'kuwa na umoja katika kukabiliana na adui wa pamoja'. Kiongozi Muadhamu amesema katika daraja ya pili, nchi za Kiislamu zinapaswa kufanya juhudi na kushirikiana katika masuala ya sayansi, utajiri, usalama na nguvu za kisiasa ili kuweza kufikia ustaarabu mpya wa Kiislamu. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiwekea lengo lake kuu kuwa ni kuifikia nukta hiyo hiyo ya ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Ayatullah Khamenei amesema masaibu ya sasa katika ulimwengu wa Kiislamu, ikiwemo kadhia ya Palestina, vita na umwagaji damu nchini Yemen, Asia Magharibi na Afrika Kaskazini yanatokana na kutofungamana na msingi wa kujiepusha kuhujumiana na kuwa na umoja katika kukabiliana na maadui wa pamoja. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema leo msiba mkubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu ni kadhia ya Palestina ambapo taifa hilo limeondolewa katika makazi yake ya jadi na kufanywa wakimbizi.

Aidha ameashiria jitihada za maadui za kupotosha maana ya sisitizo la kila mara la Imam Khomeini MA na wakuu wa mfumo wa Kiislamu kuhusu 'kondolewa Israel' na kusema: 'Sisi tunaunga mkono Palestina, uhuru na kukombolewa taifa hilo na hivyo kuondolewa Israel hakumaanishi kutimuliwa watu ambao ni Mayahudi, kwani sisi hatuna tatizo nao kama ambavyo nchini Iran kuna jamii ya Mayahudi ambao wanaishi kwa usalama kamili.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: "Watu wa Palestina, wawe ni Waislamu, Wakristo au Mayahudi ni wamiliki wa asili wa ardhi hiyo na inapasa wawe na uwezo wa kuchagua serikali yao; na maajinabi na wahuni kama Netanyahu waondoke ili Wapalestina waweze kusimamia nchi yao; na bila shaka jambo hilo litajiri tu"

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wasomi na maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu wana jukumu muhimu sana na kuongeza kuwa: "Mnapaswa kutetea haki kwa nguvu zote wala msiwaogope maadui na jueni kwamba kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, katika mustakabali usio mbali ulimwengu wa Kiislamu utashuhudia kuthibiti kwa matarajio yake yaliyojaa nuru."

3857290

captcha