IQNA

Mkutano wa 33 wa Umoja wa Kiislamu wamalizika Tehran

14:26 - November 17, 2019
Habari ID: 3472218
TEHRAN (IQNA) – Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umemalizika mjini Tehran Jumamosi usiku.

Akihutubu katika kikao hicho, Ayatullah Ibrahimi Raisi, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa dhana kuwa nchi za Magharibi ndio walinzi wa haki za binadamu na kueleza bayana kuwa, Uislamu ndio umelinda na kuheshimu kikamilifu haki za binadamu.

Aliongeza kuwa, "Hii leo, haki za binadamu kwa mujibu wa Uislamu ndizo tu zinazoweza kutoa dhamana ya kuhehimiwa haki hizo." 

Amesema nchi za Magharibi zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu, ndio wakiukaji wakubwa wa haki hizo. Amesema Uislamu ndio una dalili na hoja za wazi juu ya masuala ya haki za binadamu na ambazo zinatekelezeka.

Kadhalika amezitaka nchi za Kiislamu kuimarisha umoja na mshikamano wao, sambamba na kuboresha uhusiano wao wa kiutamaduni, kijamii na kiuchumi.

Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza Alkhamisi hapa mjini Tehran kwa kaulimbiu ya "Umoja wa Umma wa Kiislamu katika Kulinda Msikiti wa al Aqsa". Mkutano huo ulihudhuriwa na wasomi, wanasiasa, wahadhiri wa vyuo vikuu na wanafikra 400 kutoka nchi 90 duniani.   

Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu kila mwaka huandaa Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu katika Wiki ya Umoja wa Waislamu.

3469894

captcha