IQNA

Bunge la Iraq lakubali ombi la waziri mkuu kujiuzulu

14:54 - December 02, 2019
Habari ID: 3472250
TEHRAN (IQNA) Bunge la Iraq lililokutana kwa kikao cha dharura kilichofanyika Jumapili limeukubali uamuzi uliochukuliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Adil Abdul-Mahdi wa kujiuzulu wadhifa wake huo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na akthari ya wabunge, kwa kutumia kifungu cha 75 cha katiba, bunge la Iraq sambamba na kukubaliana na uamuzi huo wa Abdul-Mahdi, limemtaka Rais Barham Salih awasilishe bungeni jina la kiongozi mpya wa serikali.

Siku ya Ijumaa, Adil Abdul-Mahdi alieleza katika taarifa maalumu aliyotoa kwamba, kutokana na hali iliyopo na ili kuepusha kuendelea machafuko yanayojiri nchini humo kutokana na maandamano ya upinzani ya wananchi, analitaka Bunge lichukue uamuzi kuhusiana na kuundwa serikali mpya. Abdul-Mahdi aliwasilisha barua yake rasmi ya kujiuzulu kwa Bunge Jumamosi usiku.

Katika kikao cha leo cha bunge, Spika Muhammad al-Halbousi alisema, kulingana na kifungu cha 76 cha katiba, Rais ana fursa ya muda wa mwezi mmoja kuwasilisha bungeni jina la waziri mkuu mpya.

Katika muda huo wa mwezi mmoja hadi litakapowasilishwa bungeni jina la waziri mkuu mpya, serikali ya Adil Abdul-Mahdi itafanya kazi kama serikali ya muda. Baada ya kupita muda wa mwezi mmoja, kulingana na kifungu cha 81 cha katiba ya Iraq, endapo rais atashindwa kumpata mtu anayefaa, ni yeye mwenyewe ndiye atakayefanya kazi za waziri mkuu hadi atakapopendekezwa mtu mpya wa kushika wadhifa huo.   

Wimbi la pili la maandamano lilianza katika maeneo mbalimbali nchini Iraq tangu Oktoba 25 mwaka huu na yangali yanaendelea hadi sasa. Wizara ya Ulinzi ya Iraq Jumapili wiki hii ilitangaza kuwa upande wa tatu unahusika katika mauaji na kuwashambulia waandamanaji na vikosi vya usalama kwa lengo la kuibua machafuko na migawanyiko huko Iraq. 

3860951

captcha