IQNA

Mawaziri wa utawala wa Bouteflika wafungwa jela Algeria

18:19 - December 10, 2019
Habari ID: 3472266
TEHRAN (IQNA) – Mahakama nchini Algeria imewahukumu vifungo vya muda mrefu jela mawaziri wakuu wawili wa zamani wa nchi hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Ahmed Ouyahia amehukumiwa kifungo cha miaka 15 na faini ya dola 16,000 na Abdelmalek Sellal kifungo cha miaka 12 jela na faini ya dola 8,000 kwa kupatikana na hatia zinazohusiana na ufisadi na kuchangia kwa siri kampeni za rais aliyejiuzulu wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika.

Aidha jaji wa kesi hiyo iliyotajwa na vyombo vya habari vya Algeria kuwa ni ya kihistoria, ameamuru kutaifishwa mali na milki zote za Ouhahia na Sallal.

Mahakama hiyo pia imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela waziri wa zamani wa viwanda wa Algeria, Abdeslam Bouchouareb bila yaye kuwepo mahakamani na imeitaka Polisi ya Kimataifa kumtia nguvuni.

Mawaziri wengine wa zamani watatu wa Algeria pia wamehukumiwa vifungo vya baina ya miaka 5 hadi kumi kwa hatia zinazohusiana na ufisadi, rushwa, kutumia vibaya madaraka na kupata utajiri kwa njia zisizo za kisheria.

Baadhi ya watu waliokuwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Sidi M'Hamed mjini Algiers walishangilia na kupongeza uamuzi huo.

Hii ni mara ya kwanza kuhukumiwa waziri mkuu wa zamani nchini Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1962.

Mwezi Septemba pia Mahakama ya kijeshi ya Algeria ilimuhukumu ndugu wa kiume wa rais wa zamani wa nchi hiyo  Bouteflika, kifungo cha miaka 15 jela pamoja na watuhumiwa wenzake wengine watatu.

Saïd Bouteflika alikuwa mtu wa karibu mno kwa kaka yake Bouteflika na anahesabiwa kuwa ndiye aliyeshika madaraka ya Algeria baada ya kaka yake kupigwa na kiharusi mwaka 2013.

Tangu baada ya aliyekuwa rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika kulazimishwa na wananchi kujiuzulu tarehe 2 Aprili mwaka huu, Waalgeria wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kufutwa kazi maafisa wa kipindi cha utawala wake waliosalia madarakani.

/3470078

captcha