IQNA

Kikao cha kimataifa cha Fiqhi Oman chajadili kuhusu utunzwaji maji

16:30 - December 11, 2019
Habari ID: 3472270
TEHRAN (IQNA)- Mkutano wa 15 wa Kimataifa wa Sayansi za Fiqhi umefanyika hivi karibuni katika mji mkuu wa Oman, Muscat ambapo mada kuu ilikuwa ni kuhusu maji.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, maudhui hiyo imejadiliwa chini ya anuani ya "Fiqhi ya Maji katika Sheria za Kiislamu" ambapo wanazuoni na wanafikra 55 kutoka nchi mbali mbali wameshiriki katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini Oman.

Kongamano hilo ambalo limefanyika kwa uongozi wa Mufti Mkuu wa Oman Sheikh Ahmed bin Hamad al Khalili limemalizika kwa kutoa wito wa kuhuishwa Sira ya Mtume Muhammad SAW ambaye aliwahimiza watu kuzingatia utunzwaji maji na mimea. Aidha washiriki wametaka kuchukuliwe hatua imara kwa lengo la kulinda maji na pia kukurubisha mataifa, jamii na watu binafsi.

Halikadhalika kongamano hilo limesema jamii za Waislamu zina jukumu la kidini la kulinda na kutunza maji, kutumia maji kwa njia sahihi, na kuzuia uchafuzi wa maji. Halikadhalika jamii za Waislamu zimetakiwa  kuhakikisha uadilifu wa kijamii unatekelezwa kwa kuwafikishia wote maji. 

Mkutano wa 15 wa Kimataifa wa Sayansi za Fiqhi pia umetoa wito kwa wanasayansi na taasisi zote husika kuanzisha mkakati maalumu wa kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji ni endelevu na vinadumu ili kuhudumia jamii. Aidha mkutano huo umetambua jitihada za Oman za kupanda mitende  milioni moja katika mkakati ulioanzishwa na kiongozi wan chi hiyo, Sultan Qaboos.

Kikao hicho cha Muscat pia kimetaka wahubiri wa Kiislamu wapewe mafunzo kuhusu masuala ya utunzaji wa maji kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.

3863401

captcha