Rais Rouhani ameyasema hayo mapema leo kabla ya kuondoka mjini Tehran akielekea Malaysia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Kuala Lumpur 2019. Amesema kuwa, mkutano huo utajadili uhusiano wa pande kadhaa katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Vilevile ameashiria uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu katika masuala mbalimbali ya kijiografia, nishati, jamii kubwa ya watu, viwanda, utamaduni na ustaarabu na kusema: Ugaidi, vita, umwagaji damu, uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi nyingine na kutokuwepo mazingira mazuri ya ustawi ni miongoni matatizo ya sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Rouhani amesema kuwa, Iran na Malaysia zina misimamo inayofanana kuhusiana na masuala mengi ya kikanda na Ulimwengu wa Kiislamu na zina mtazamo mmoja kuhusiana na udharura wa kuwepo mazungumzo kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi masuala ya Waislamu.
Vilevile ameashiria uhusiano wa Iran na Japan katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na masuala ya mazingira na akasema: Vikwazo vya kidhalimu na vilivyo kinyume na sheria vya Marekani dhidi ya Iran havitadumu na hapana shaka kuwa, nchi nyingi duniani zinataka kuwa na uhusiano mwema na Jamhuri ya Kiislamu.