IQNA

Saudia yakasirishwa na Malaysia kualika viongozi wa nchi za Kiislamu

18:10 - December 24, 2019
Habari ID: 3472300
TEHRAN (IQNA) –Hatua ya Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Mohamad kuwa mwenyeji wa kikao cha viongozi wa nchi za Kiislamu imeikasirisha Saudia Arabia na waitifaki wake.

Duru za kidiplomasia zinadokeza kuwa, Saudi Arabia imekerwa sana hasa kutokana na kuwa wakosoaji wake wakubwa yaani Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Amiri wa Qatar Sheikh Tamim Hamad Al Thani na Rais Hassan Rouhani wa Iran walialikwa na kuhudhuria kikao hicho.

Qatar, Iran na Uturuki zimeimarisha uhusiano wao na ni wakosoaji wakuu wa ubabe wa ufalme wa Saudi Arabia katika eneo. Qatar inakabiliwa na mzingiro unaaongozwa na Saudi Arabia tokea mwaka 2017 na moja ya sababu ya kuwekewa mzingiro huo ni uhusiano wake wa karibu na Iran pamoja na harakati za Hizbullah na Hamas. Uhusiano wa Uturuki na Saudi Arabia nao ulivurugika baada ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Saudia, Jamal Khashoggi, kuuawa katika Ubalozi Mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018.  Iran nayo imekuwa na msuguano na Saudia kwa muda mrefu hasa kutokana na hatua ya Iran kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina, Ansarullah ya Yemen na pia kuunga mkono serikali ya Syria katika vita vyake dhidi ya magaidi. 

Saudia imelaani kikao hicho cha Kuala Lumpur 2019 na ilizichochea nchi kadhaa zisihudhurie kikao hicho. Nchi kama vile Kuwait, Bahrain, Pakistan na UAE zilikataa kutuma wawkilishi katika kikao hicho kufuatia mashinikizo ya Saudia. Imedokezwa kuwa Mfalme Salman bin Abdul Aziz al Saud alimpigia simu Mahathir Muhamad na kubainisha wazi kuwa hakufurahishwa na kikao hicho.

Kikao hicho cha Kuala Lumpur 2019 kilifanyika Disemba 19-21 na kilijadili masuala muhimu yanayowahusu Waislamu duniani kama vile matatizo ya wakimbizi Waislamu, chakula, utambulisho wa kitaifa na kiutamaduni, chuki dhidi ya Uislamu, teknolojia, biashara, intaneti na usalama. Mfalme Salman alimfahamisha Waziri Mkuu wa Malaysia kuwa anahisi 'masuala kama hayo yanapaswa kujadiliwa tu na OIC.'

Mahathir Muhamad amekanusha madai kuwa kikao hicho kililenga kuibua mgawanyika OIC na kusema wapinzani hawakufahamu nia ya Malaysia.

3866282/

captcha