Akizungumza katika sherehe ya kumuarifisha kama katibu mkuu wa jumuiya hiyo na kumuaga katibu mkuu anayeondoka, Hujjatul Islam Shahriyari ameongeza kuwa Waislamu pia wanapaswa kutumia uwezo wao mkubwa kukabiliana na madola ya kiistikbari na kibeberi. Katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Tehran Jumatano, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ameashiria mpango wake wa kuimarisha umoja na ukuruba miongoni mwa Waislamu na kusema atazingatia vipaumbele ambavyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alimpa wakati wa kumteua.
Wiki mbili zilizopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alimteua Hujjatul Islam Hamid Shahriyari kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika dikrii amemteua katibu mkuu mpya wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na kuelezea matumaini yake kuwa, kutapatikana taufiki kwa kuendelezwa jitihada ambazo zimekuwa zikitekelezwa na wasimamizi waliotangulia wa jumuiya hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema inatazamiwa kuwa, Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu itatumia busara ya Kiislamu pamoja na wanafikra na wasomi katika Ulimwengu wa Kiislamu hasa vijana katika kuchukua hatua za kukukuribisha kifikira na kivitendo madhehebu za Kiislamu na kwa msingi huo kujenga upya harakati iliyoanza miongo kadhaa iliyopita. Aidha kiongozi muadhamu ametoa shukrani zake za dhati kwa katibu mkuu anayeondoka, Hujjatul Islam Muhsin Araki kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake.
Inafaa kuashiria hapa kuwa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ilianzishwa mwaka 1990 kufuatia dikrii ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuleta umoja, maelewano na ukuruba baina ya madhehebu za Kiislamu. Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu inafuatilia malengo ya Darul Taqrib iliyokuwa Cairo, Misri na ambayo ilididimia baada ya kuaga dunia maulamaa walioiasisi taasisi hiyo ya umoja wa Kiislamu.
3470190