IQNA

Hamas yasisitiza haitalegeza msimamo mbele ya utawala wa Israel

11:23 - December 30, 2019
Habari ID: 3472316
TEHRAN (IQNA) - Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amepinga kulegeza misimamo mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kutoa suhula mbalimbali huko Ghaza mkabala na Hamas kusitisha uvurumishaji wa makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Suhail al Hindi ameeleza kuwa habari zilizotangazwa na duru za habari za Israel kwamba itatoa huduma za vifaa mbalimbali huko Ghaza iwapo Hamas itaacha kuvurumisha makombora kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hazina msingi wowote. 

Mwakilishi wa Hamas amekanusha taarifa hizo za utawala wa Kizayuni baada ya kuvurumishwa Jumatano iliyopita kombora kuelekea katika kitongoji cha Asqalan kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu wakati Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni akihutubia. 

Netanyahu ambaye alielekea katika kitongoji hicho kwa ajili ya kutoa hotuba na kampeni za uchaguzi alilazimika kuondoka huko na kupelekekwa kusikojulikana baada ya kuvurumishwa kombora. 

Kuvurumishwa kombora hilo kumewatia kiwewe na woga Wazayuni wakihofia maisha yao na kuwapelekea viongozi wengi wa utawala huo kwa mara nyingine kuyatishia makundi ya muqawama kwamba wataanzisha siasa za kuwaua kigaidi viongozi wa Hamas ikiwa ni katika kujibu uvurumishaji huo wa kombora. 

Hivi karibuni Hamas alibaini wazi kuwa, mapambano ya pande zote na kwa kutumia mbinu na nyezo zote ndiyo chaguo la taifa la Palestina kwa ajili ya kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel.

Abdullatif al-Qanou alisema katika maadhimisho ya mwaka wa 32 wa kuanza Intifadha ya kwanza ya Wapalestina iliyopewa jina la Intifadha ya Jiwe kwamba mapambano ya Intifadha yamehuisha moyo wa kujitolea wa taifa la Palestina kwa ajili ya kukabiliana na Wazayuni maghasibu.

Al Qanou amesisitiza udharura wa kuendelezwa mapambano ya ukombozi wa Palestina ya Intifadha na kusema kuwa, maandamano ya Haki ya Kurejea yanayofanywa kila siku ya Ijumaa ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuvunjwa mzingiro wa Israel dhidi ya wakazi wa eneo hilo ni baadhi ya nyenzo zinazotumiwa na Wapalestina katika mapambano yao dhidi ya utawala haramu wa Israel.

/3470214

 

captcha