IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran inalaani hujuma ya Marekani huko Iraq, watu wa eneo hili wanaichukia Marekani

17:57 - January 01, 2020
Habari ID: 3472324
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinzudi ya Kiislamu akibainisha kwamba, 'Mimi, serikali na taifa la Iran tunalaani vikali shambulizi la Marekani dhidi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq', amesisitiza kuwa, watu wa eneo hili wanaichukia sana Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran alipokutana na maelfu ya madaktari kutoka maeneo yote ya Iran, na kubainisha kwamba wimbi la kuchukiwa Marekani katika eneo hususan nchini Iraq, ni radiamali ya kawaida ya wananchi kutokana na jinai za Marekani. Ameongeza kwamba kwa hakika shambulizi la Marekani dhidi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq ni ulipizaji kisasi wa Marekani kwa kushindwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) kwani wanamuqawama hao wa Hashdu sh-Sha'abi ndio waliolitokomeza genge hilo. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei pia ameashiria matamshi ya rais wa Marekani ya kuitwisha lawama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa eti ni muhusika mkuu wa kadhia ya siku ya jana Jumanne nchini Iraq na vitisho vyake kwa taifa la Iran, na kusisitiza kwamba, Marekani imekosea kwa kuwa suala hilo halihusiani na Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa, wote wanapaswa kufahamu kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki vita, lakini mtu yeyote anayetishia maslahi, izza, adhama na maenendeleo ya taifa la Iran, atakabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa nchi hii bila kuchelewa. Kadhalika Ayatullah Khamenei ameendelea kwa kusema: " Watu wa nchi za eneo hili wanaichukia Marekani. Ni kwa nini Wamarekani hawafahamu hili? Nyini Wamarekani mumetenda jinai Afghanistan na Iraq. Katika zama za awali baada ya kupinduliwa Saddam, Marekani hususan kupitia idara khabithi ya 'Black Water' iliua zaidi ya wasomi 1000 Wairaqi na pia raia wa kawaida. Huko Afghansitan pia, Marekani imeshambulia kwa mabomu mara kadhaa misafara ya harusi na pia vikao vya maombolezo. Marekani imetanda jinai dhidi ya watu wa Iraq, Afghanistan, Syria na maeneo mengine na hivyo watu wanaichukia Marekani sana na inafika wakati chuki hii inajitokeza wazi na hili halihusiani na Iran."

3868100

 

captcha