IQNA

Maandamano yaendelea India kupinga sheria ya uraia inyaowabagua Waislamu

10:48 - January 02, 2020
Habari ID: 3472327
TEHRAN (IQNA) – Maelfu ya watu wa India wameukaribisha mwaka mpya wa 2020 Miladia kwa maandamano ya kupinga sheria ya uraia inayowabagua Waislamu.

Maandamano hayo yameendelea kwa wiki tatu mfululizo licha ya jitihada za kuyakandamiza za Waziri Mkuu Narendra Modi.

Sheria hiyo mpya ya uraia inaruhusu kupatiwa uraia wahajiri wa jamii za Wahindu, Mabudha na hata Wakristo wanaotokea katika nchi jirani za Pakistan, Bangladesh na Afghanistan, huku ikizuia kupewa uraia Waislamu wanaotoka katika nchi hizo.

Karibu watu 30 wameuawa katika maandamano ya kupinga sheria hiyo ambayo yalianza Disemba 12 huku mamia ya wengine wakijeruhiwa. Polisi nchini India wanalaumiwa kutumia nguvu ziada na mabavu kuwakandamiza watu wanaoandamana kupinga sheria hiyo inayowabagua Waislamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuwatetea na kuwahami Waislamu wa India.

Shah Mehmood Qureshi amewaambia waandishi habari huko Multan katika jimbo la Punjab kwamba: Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inalazimika kuwakusanya pamoja mawaziri wa mashauri ya kigeni wa nchi za Kiislamu kwa shabaha ya kutetea haki za Waislamu nchini India kupitia njia ya kupinga sheria mpya ya uraia nchini humo.

Itakumbukwa kuwa tarehe 24 mwezi huu wa Disemba Kamisheni Huru ya Kudumu ya Haki za Binadamu ya OIC ilitoa taarifa ikilaani ukatili na mauaji yaliyofanyika nchini India katika maandamo yanayopinga sheria mpya ya uraia. Kamisheni hiyo iliitaka jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuishinikiza serikali ya New Delhi ili ifute vipengee vinavyowabagua Waislamu katika sheria mpya ya uraia na kuheshimu vigezo vya kimataifa wakati wa kukabiliana na waandamanaji.

3470240

captcha