IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kisasi kikali kinawasubiri waliomuua shahidi Jenerali Suleimani, siku tatu za maombolezo Iran

12:08 - January 03, 2020
Habari ID: 3472329
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametuma salamu za rambirambi kutokana na kuuliwa shahidi Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Suleimani na kusema kuwa: Kisasi kikali kinawasubiri watenda jinai ambao mikono yao michafu imemwaga damu yake na mashahidi wengine katika shambulizi la usiku wa kuamkia leo.

Ayatullah Ali Khamenei amesema katika ujumbe huo kwamba: Hatimaye SUlaimani kipenzi amepata daraja hiyo ya juu na damu yake safi imemwagwa na mtu muovu kupita wote baada ya miaka mingi ya kupigana jihadi kwa ikhlasi na ushujaa katika medani za kupambana na mashetani na waovu wa dunia na baada ya miaka mingi ya hamu ya kupata daraja ya juu ya kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu."

Ameongeza kuwa: "Kuuliwa kwake shahidi ni malipo ya juhudi kubwa ambazo hazikuwa na kikomo za Meja Jenerali Shahidi Soleimani katika miaka yote iliyopita na kuondoka kwake hakutasitisha na kufunga kazi na njia yake." 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Shahidi Qassem Suleimani alikuwa kinara wa kimataifa wa kambi ya mapambano, na wanamuqawama wote watalipiza kisasi cha damu yake. Ameongeza kuwa: "Marafiki na vilevile maadui wanapaswa kuelewa kwamba, njia ya kupigana jihadi na mapambano itaendelea kwa ari na moyo mkubwa zaidi, na ushindi wa mwisho unawasubiri wapigaji jihadi katika njia hii iliyobarikiwa." 

 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kuondoka kwa kamanda aliyesabilia kila kitu na kipenzi chetu kunauma, lakini kuendelea kwa mapambano hadi utakapopatikana ushindi wa mwisho kutatia shubiri katika vinywa vya makatili na watenda jinai. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Taifa la Iran litaendelea kumkumbuka na kumuenzi shahidi Qassem Solaimani na mashahidi wengine waliokuwa pamoja naye hususan mpigana jihadi mkubwa wa Uislamu, Abu Mahdi al Muhandes, kwa sababu hiyo ninatangza siku tatu za maombolezo ya taifa.

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Luteni Jenerali Qassem Solaimani na naibu mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hasdul Shaabi, Abu Mahdi al Muhandes wameuawa shahidi mapema leo Ijumaa katika shambulizi la roketi lililofyatuliwa na helikopta ya Marekani katika barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.  

/3868486/

captcha