IQNA

Mwili mtoharifu wa Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani waingia Iran

12:54 - January 05, 2020
Habari ID: 3472336
TEHRAN (IQNA) - Mwili mtoharifu wa Shahidi Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) umewasili katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo asubuhi katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Ahwaz kusini mwa nchi.

Idadi kubwa ya watu wamefika katika uwanja huo wa ndege kuupokea mwili wa Shahidi Qassem Suleimani na ule wa Abu Mahdi la Muhandis, Kamanda wa Kikosi cha Hashd al Shaabi cha Iraq pamoja na wanajihadi wenzao waliouawa Ijumaa katika hujuma ya kigaidi ya Marekani mjini Baghdad.

Siku ya Jumamosi kulifanyika maandamano ya mazishi ya mashahidi hao katika miji ya Kadhimein, Baghdad, Karabala na Najaf nchini Iraq.

Kwa mujibu wa ratiba, leo mjini Ahavaz, mkoani Khuzestan, kutafanyika shughuli ya mazishi na kuwaaga mashahidi hao wa muqawama.

Baadaye leo adhuhuri shughuli ya mazishi itaendelea katika Haram Takatifu ya Imam Ridha AS, Imam wa nane wa Mashia katika mji wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran. Miji mingine ambayo kutafanyika shughuli ya mazishi na kuwaaga mashahidi hao ni Tehran, Qum na hatimaye maziko yamepengwa kufanyika Kerman alikozaliwa Shahidi Luteni Jenerali Soleimani.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani na naibu mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hashdul Shaabi, Abu Mahdi al Muhandes waliuawa shahidi mapema Ijumaa katika shambulizi la Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetangaza kuwa, Rais Donald Trump wa nchi hiyo ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa shahidi Jenerali Qassem Soleimani.  

3869245

captcha