IQNA

Waislamu Kodivaa wamkumbuka Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani

11:31 - January 15, 2020
Habari ID: 3472373
TEHRAN (IQNA) - Waislamu wa Ivory Coast wamefanya kikao cha kumuenzi na kumkumbuka Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mashahidi wenzake waliouawa hivi karibuni na askari magaidi wa Marekani nchini Iraq.

Kikao hicho cha kumuomboleza Jenerali Soleimani na mashahidi wenzake kilifanyika usiku wa kuamkia jana Jumatatu katika Msikiti wa Ithnaashari katika eneo la Markouri ulioko katika mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo Abidjan.

Washiriki wa kikao hicho wametuma salamu za rambirambi kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, serikali na taifa la Iran kwa ujumla, kwa kuondokewa na shujaa huyo wa muqawama.

Aidha wametoa mkono wa pole kwa makundi na harakati zote za muqawama kote duniani, kwa kuuliwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, na mashahidi wenzake.

Waislamu wa Kodivaa walioshiriki mkutano huo katika Msikiti wa Ithnaashari mjini Abidjan wamemtaja Haji Soleimani kama shujaa na mwanamapambano aliyesabilia maisha yake katika harakati na jitihada za kuyatokomeza makundi ya kigaidi hususan Daesh (ISIS) katika eneo la Asia Magharibi.

Kadhalika washiriki wa kikao hicho wakiwemo waandishi wa habari mashuhuri wa Ivory Coast wameilaani Marekani kwa kutekeleza ugaidi huo dhidi ya Soleimani, na kisha kuihadaa dunia kwa kujaribu kuhalalisha jinai hiyo.

Wiki iliyopita, kundi la Maimamu wa Kisunni na Kishia pamoja na wanafunzi na wanachuo nchini Ivory Coast walikusanyika katika ubalozi wa Iran nchini humo, kutoa mkono wa pole kwa taifa la Iran kufuatia mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani katika ardhi ya Iraq.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Ijumaa Alfajiri 3 Januari aliwasili nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo. Punde baada ya kuwasili, akiwa ndani ya gari pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashd al Shaabi pamoja na watu wengine wanane, walishambuliwa tokea angani na wanajeshi vamizi na wa kigaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na wote wakauawa shahidi katika tukio hilo.

Kufuatia ugaidi huo wa Marekani usiku wa kuamkia Jumatano 8 Januari, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilizipiga kwa makumi ya makombora, kambi mbili za Marekani nchini Iraq ikiwa ni kujibu jinai ya kigaidi iliyofanywa na askari vamizi wa Marekani ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.

83632006

captcha