IQNA

Upinzani mkali kuhusu mpango wa 'Muamala wa Karne'

17:57 - January 28, 2020
Habari ID: 3472412
TEHRAN (IQNA) – Rais wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amezitaka nchi za Kiislamu na Kiarabu kususia uzinduzi wa mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na mgogoro wa Palestina uliopewa jina la "Muamala wa Karne".

Mahmoud Abbas amesema kuwa, anapinga aina yoyote ya mapatano yanayopendekezwa katika mpango huo wa Trump.

Msemaji wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Nabil Abu Rudeineh amesema mabalozi na wawakilishi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu walioalikwa kushiriki katika uzinduzi wa mpango huo huko Washington wameombwa kususia uzinduzi wake kwa sababu Wapalestina wanaamini kwamba, ni njama ya kukandamiza haki zao na kukwamisha uundaji wa dola huru la Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.

Wakati huo huo Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amewaambia wajumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kwamba, amepokea vitisho vya kulipa gharama kubwa baada ya kukataa kupokea simu ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyetaka kuzungumzia mpango huo wa Muamala wa Karne.

Ni vyema kusema hapa kuwa, vyama na makundi ya Palestina yamekariri upinzani wao kwa mpango uliotayarishwa na Marekani na Israel. 

Makundi ya mapambano ya uhuru ya Palestina yametangaza kuwa, siku Trump atakapotangaza mpango huo wa kishetani wa Muamala wa Karne itapewa jina la "Siku ya Ghadhabu ya Taifa." Vilevile yametoa wito wa kususiwa bidhaa za Marekani. 

Katika upande mwingine Katibu Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) Saeb Erekat amesema kwamba Wapalestina watajiondoa katika vipengee muhimu Makubaliano ya Oslo iwapo Trump atazindua rasmi mpango wake wa Muamala wa Karne.

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema madhumuni ya njama za Marekani dhidi ya Wapalestina kwa jina la 'Muamala wa Karne' ni kuwadhalilisha na kuwatweza Waislamu.

Akihutubia kikao rasmi cha Bunge la Iran mapema leo, Dakta Ali Larijani amesema Marekani imepata uthubutu wa kuzindua njama zake hizo batili kutokana na mgawanyiko ulioko miongoni mwa Waislamu.

Huku akiashiria maandamano ya wananchi wa Iraq dhidi ya Marekani, Dakta Larijani amesema muda si mrefu Wamarekani wataelewa na kushuhudia matokeo ya njama zao hizo chafu zinazokusudia kuhalalisha jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Leo Jumanne, rais wa Marekani, Donald Trump amepanga kuuzindua mpango huo baada ya kuonana na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu na Benny Gantz, mkuu wa Muungano wa Blu na Nyeupe wa utawala huo pandikizi.

Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.  

3874942

captcha