IQNA

Maombolezo ya kukumbuka siku alipokufa shahidi Bibi Fatimatu-Zahra SA yafanyika Iran

12:35 - January 29, 2020
Habari ID: 3472416
TEHRAN (IQNA) - Umati mkubwa wa wananchi Waislamu wa Iran leo umeshiriki nchini kote kwenye maombolezo ya kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatimatu-Zahra SA binti kipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na mke wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib AS, Imamu wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Leo Jumatano, tarehe tatu Mfunguo Tisa Jamadi-Thani 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 29 Januari 2020 miladia wapenzi na maashiki wa Ahlul-Bayt wa Mtume SAW wamehudhuria misikitini, kwenye hussainiyya na maeneo mengine ya kidini, ikiwa ni pamoja na katika haram tukufu ya Imam Ridha (as), Imam wa nane wa Waislamu wa Kishia iliyoko katika mji wa Mashhad, kusini mashariki mwa Iran na katika haram ya mtukufu Bibi Maasumah (sa) iliyoko mjini Qum kusini mwa Tehran kuomboleza kufa shahidi kidhulma kwa binti mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Maombolezo ya kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatima Zahra SA yamefanyika mjini Tehran katika Husseiniya ya Imam Khomeini MA na kuhudhuriwa pia na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, maafisa wa ngazi za juu nchini na wananchi.
Chini ya malezi ya baba yake, Bibi Fatima alifikia daraja la juu katika maarifa, elimu na uchamungu. Katika maisha yake, Bibi huyo mtukufu alifahamika sana kwa ukarimu, kujitolea, subira, uchamungu na kuwasaidia masikini na watu wasiojiweza.
Mtukufu huyo alijulikana kwa lakabu na majina kadhaa ya sifa teule kama Zahra, Siddiqah, Taahirah, Mubaarakah, Batul, Raadhiyah na Mardhiyyah.

3875017

captcha