IQNA

Ismail Haniya

Wapalestina hawatawasamehe wanaounga mkono 'muamala wa karne'

19:45 - January 30, 2020
Habari ID: 3472422
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano (Muqawama) ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniyeh ametuma ujumbe kwenda kwa viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu akionya ushiriki wa aina yoyote kwa ajili ya kutekelezwa au kuukubali mpango wa Muamala wa Karne na kubainisha kuwa hilo ni kosa kubwa ambalo kamwe raia wa Palestina hawatalisamehe.

Katika ujumbe huo Haniyeh amewataka viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kuupinga mpango huo unaodhamini maslahi ya utawala wa Kizayuni. Kadhalika ametaka kuchukuliwe msimamo imara mkabala wa upendeleo wa wazi wa serikali ya Marekani na njama chafu za utawala wa Kizayuni pamoja na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi. Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa upuuzaji kuhusu 'Muamala wa Karne' na ushiriki katika kufanikisha au kukubali kutekelezwa kwake, itakuwa fedheha ambayo kamwe haitofutika milele.

Akiashiria uwepo wa umoja wa safu za Wapalestina katika kukabiliana na mpango huo, amesema kuwa amekubaliana na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na uetekelezwaji wa mpango tajwa. Jumanne iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika ikulu ya White House, alizindua mpango wa kibaguzi uliopewa jina la "Muamala wa Karne" akidai kuwa ni fursa ya kutatua mgogoro wa Wapalestina na Israel.

Rais Donald Trump wa Marekani na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel katika mpango huo walilihesabia suala la hitilafu za nchi za Kiarabu katika vipengee na hata utekelezwaji wa mpango wa Muamala wa Karne kwa ajili ya kufikia malengo yao. Hata hivyo, pamoja na kuwa, Trump na Netanyahu wamepuuza uwezo wa mataifa ya Kiislamu, lakini hawajafanya tathmini sahihi kuhusiana na uwezo wa makundi ya muqawama na mapambano katika eneo la Asia Magharibi.

3875267

captcha