IQNA

Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu yapinga 'muamala wa karne'

16:51 - February 03, 2020
Habari ID: 3472436
TEHRAN (IQNA) - Katibu wa Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu amesema kuwa, Palestina ndio mpaka wa ulimwengu wa Kiislamu na kwamba suala la kuilinda na kuihami Palestina ni wajibu wa Kiqur'ani wa kila Muislamu.

Sheikh Hamid Hawali Shahriari alizungumza hayo jana (Jumapili) na huku akigusia mpango wa Kimarekani-Kizayuni wa "Muamala wa Karne" amesema, marais wa Marekani daima wanatumikia lobi za Wazayuni na ni kwa njia hiyo ndipo wanapoweza kuendelea na tawala zao za kishetani.

Vile vile amesema, kwa njama zake hizi mpya, sasa hivi Marekani imekanyaga haki za kimsingi kabisa za Wapalestina na hilo linazidi kuonesha dhati ya kihayawani na kikatili ya viongozi wa Marekani.

Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Palestina imetangaza kuwa, ni haramu kushiriki katika utekelezaji wa mpango wa kibaguzi uliopendekezwa na Marekani na Wazayuni kwa ajili ya kadhia ya Palestina.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulama wa Palestina, Marwan Abu Ras amewataka wanazuoni wa Umma wa Kiislamu pia kutoa fatwa ya kupinga "Muamala wa Karne" na kuisambaza kwa wafuasi wao.

Abu Ras ameongeza kuwa, mpango huo wa Muamala wa Karne ni jinai kubwa dhidi ya taifa la Palestina na Baitul Muqaddas, na kukabiliana nao ni wadhifa na jukumu la kidini na kitaifa.

Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu ya Palestina pia imetangaza kuwa, kuboresha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ni sawa na kufanya jinai dhidi ya taifa la Palestina. 

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa mpango huu wa Rais Donald Trump wa Marekani unapingana na hati ya Umoja wa Mataifa na vilevile maazimio ya Baraza la Usalama la umoja wa huo kuhusiana na Palestina. Mpango huo ambao ni muamala baina ya Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na hauutambui upande wa Palestina ambao ndio mmiliki halisi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ni muamala wa kisiasa wenye lengo la kuwaokoa wanasiasa hao wawili wanaokabiliwa na kashfa na migogoro mingi ya ndani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba kile kinachotajwa kuwa 'Muamala wa Karne' kwa hakika ni 'Hiana na Usaliti' dhidi ya taifa la Palestina.

3874341

captcha