IQNA

Umoja wa Afrika wapinga mpango wa Trump kuhusu Palestina

19:33 - February 09, 2020
Habari ID: 3472455
TEHRAN (IQNA) - Viongozi wa Afrika wameulaani mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambao ni maarufu kama 'muamala wa karne' kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Israel na Palestina na kuutaja kuwa usio na uhalali.

Akizungumza na viongozi wakuu wa mataifa ya Afrika kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika ulioanza leo mjini Addis Ababa, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja huo, Moussa Faki Mahamat, amesema mpango huo uliotangazwa mwishoni mwa mwezi uliopita unawakilisha uvunjaji usio kipimo wa maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Mahamat, ambaye alitumia hotuba yake hiyo kurejelea mshikamano wa Afrika na malengo ya ukombozi wa taifa la Palestina, alisema mpango wa Trump uliandaliwa bila kushauriana na jamii  ya kimataifa, na kwamba unazikanyaga haki za Wapalestina.

Mpango huo uliopewa jina la 'muamala wa karne', ulikataliwa tangu mwanzoni na Wapalestina wakiungwa mkono na jamii ya kimataifa na mataifa jirani ya eneo la Asia Magharibi,  ulimwengu wa Kiislamu na hata idadi kubwa ya wajumbe wa chama cha upinzani cha Democrat katika Bunge la Kongresi la Marekani.

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, ambaye kawaida huhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika kama mgeni mwalikwa, mara hii ameshindwa kuhudhuria, huku maafisa wa serikali yake wakisema anaelekea Umoja wa Mataifa kulishinikiza Baraza la Usalama kuulaani mpango huo wa amani.

Tarehe 28 Januari, rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na waziri mkuu wa utawala bandia wa Israel, Benjamin Netanyahu alizindua mpango wa ubaguzi wa kimbari wa Muamala wa Karne.

Kuitambua rasmi Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuupatia utawala huo haramu umiliki wa asilimi 30 ya eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, kupingwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea nchini kwao na kupokonywa silaha kikamilifu ile itakayoitwa nchi ya Palestina ni miongoni mwa vipengele vya mpango huo wa udhalilishaji.

3877692

captcha