IQNA

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu asema

Luteni Jenerali Soleimani alikuwa mwenye huruma kwa watu, lakini mkali kwa maadui

11:43 - February 14, 2020
Habari ID: 3472471
TEHRAN (IQNA) - Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amemtaja Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC kama shakhsia aliyehuisha 'harakati za jihadi na kuuawa shahidi' katika ulimwengu wa Kiislamu.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo jana alasiri hapa Tehran aliposhiriki marasimu ya arubaini ya Kamanda Soleimani na Mashahidi wenzake na kusisitiza kuwa, "Jenerali Soleimani alikuwa mwenye huruma kwa wananchi na watu wa kawaida, lakini mkali kwa maadui."

Ameeleza bayana kuwa, Shahidi Soleimani alitambua vyema umuhimu wa jihadi na alienda sehemu mbalimbali alikosikia watu wanadhulimiwa, na kwa msingi huo jenerali huyo ni kiigizo chema cha kufuatwa katika kuwalinda na kuwatetea Waislamu.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena ameonya kuwa, jeshi la IRGC halitasita kutoa pigo kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel iwapo zitachukua hatua yoyote ya kipumbavu dhidi ya taifa kubwa la Iran.

Kadhalika ametoa onyo kwa waitifaki wa utawala wa Marekani ambao ni adui wa umma wa Kiislamu na kusema kwamba, wanapaswa kusitisha njama zao ili wasiwe waathirika wa sera mbovu za Washington.  

Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, mrengo wa muqawama na mapambano ya Kiislamu una azma imara ya kuendeleza mapambano yenye malengo matakatifu na kwamba mustakabali utakuwa mwema kwani kumalizika uwepo wa Marekani ni jambo ambalo litaleta  uthabiti, ustawi, usalama na mlingano katika eneo la Asia Magharibi.

Kamanda Qassem Soleimani ambaye Januari 3 mwaka huu alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi la kigaidi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.
Katika kutekeleza ahadi yake ya kulipiza kisasi kikali kwa Marekani kutokana na nchi hiyo kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na shakhsia wengine aliokuwa nao, Iran ilishambulia kwa makombora kambi ya kijeshi ya askari gaidi wa Marekani ya Ain Assad nchini Iraq hapo tarehe 8 Januari.

3878619

captcha