IQNA

Ujerumani yasambaratisha mtandao wa magaidi waliopanga kuwashambulia Waislamu

16:23 - February 15, 2020
Habari ID: 3472472
TEHRAN (IQNA) – Polisi nchini Ujerumani Ijumaa waliwakamata watu 12 ambao wanashukiwa kuanzisha mtandano wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali kwa lengo la kutekeleza hujuma dhidi ya wanasiasa, wakimbizi na Waislamu.

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ujerumani (GBA) imesema washukiwa wanne waliokamatwa walianzisha 'kundi la kigaidi' Septemba 2019 na walikuwa wanakutana mara kwa mara na kuwasiliana kwa njia ya simu na kupitia makundi ya mitandao ya kijamii. Washukiwa wengine wanane wamekamatwa kwa tuhuma za kuupa mtandano huo misaada ya kifedha na silaha.

"Lengo la mtandao huu lilikuwa ni kuutikisha na hatimaya kuuvuruga mfumo wa kidemokrasia na maelewano ya kijamii nchini Ujerumani," imesema taarifa ya GBA. "Ili kuandaa mazingira yanayofanana nay ale ya vita vya ndani, kulikuwa na mpango wa kutekeleza mashambulizi dhidi ya wanasiasa, wakimbizi na Waislamu," imebaini taarfa hiyo.

Mwaka jana serikali ya Ujerumani ilianzisha oparesheni ya kukabiliana na utumiaji mabavu na hujuma za chuki za makundi ya kisiasa ya mrengo wa kulia ambayo yanapinga kuwepo watu wasio na asilia yay a Kijerumani katika nchi hiyo.

Idara ya Usalama wa Taifa Ujerumani inaamini kuwa kuna karibu watu 24,100 wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia ya kufurutu ada na karibu nusu yao wako tayari kutumia mabavu na kutekeleza hujuma za kigaidi dhidi ya wakimbizi, raia wa kigeni, Waislamu na wanasiasa wasioafikiana na sera za mrengo huo wa kulia.

3470635

 

captcha