IQNA

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kufuatia mapatano ya Marekani na Taliban

19:00 - March 01, 2020
Habari ID: 3472520
TEHRAN (IQNA) - Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kuhusu makubaliano yaliyotiwa saini jana Jumamosi baina ya Marekani na kundi la Taliban la Afghanistan na kusisitiza kuwa, amani ya kudumu nchini humo itapatikana tu kupitia mazungumzo ya Waafghani wenyewe kwa wenyewe na kushirikishwa makundi yote likiwemo la Taliban.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetolewa leo Jumapili na kuongeza kuwa, sharti jingine la kuweza kufikiwa amani ya kudumu huko Afghanistan ni kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Tehran iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika katika juhudi za kuleta utulivu wa kudumu nchini Afghanistan, kama ambavyo inaunga mkono jitihada zozote zinazofanyika kulifanikisha jambo hilo.

Vile vile imesema, wanajeshi wa madola ajinabi yako nchini Afghanistan kinyume cha sheria na kuweko kwao nchini humo ndicho chanzo kikuu cha ukosefu wa amani na machafuko. Imeongeza kuwa, kutoka wanajeshi ajinabi nchini Afghanistan ni moja ya mashrti makuu ya kupatikana usalama nchini humo, hivyo Iran inaunga mkono juhudi zozote zinazolenga kuwaondoa wanajeshi wa madola ajinabi nchini humo.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema, hivi sasa Marekani inafanya njama za kuhalalisha uvamizi wake wa kijeshi na kuendelea kuweka wanajeshi wake huko Afghanistan kama ambavyo Washington haina nguvu za kisheria za kutia saini makubaliano ya amani wala kuamua mustakbali wa Afghanistan.

Jana Jumamosi, Marekani na kundi la Taliban zilitiliana saini makubaliano ya amani baada ya mazungumzo ya mizunguko 12 ya takriban miaka miwili. Makubaliano hayo ya amani yalitiwa saini mjini Doha Qatar yakiwa yamefuatiwa na wiki moja ya kupunguza mapigano baina ya pande hizo mbili nchini Afghanistan.

3882345

captcha