IQNA

Ismail Haniya: Russia inapinga muamala wa karne

7:37 - March 04, 2020
Habari ID: 3472528
TEHRAN (IQNA) – Kiongozi wa Harakati ya Mapmbano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniya amesema Russia inapinga mpango wa 'muamala wa karne' uliowasilishwa na Mareknai kuhusu kadhia ya Palestina.

Amesema Russia imepinga mpango huo kutokana na kuwa unakiuka sharia na kanuni za kimataifa.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa wa Hamas pia ametupilia mbali ombi la Marekani la kutaka Washingto iwe na uhusiano wa kisiasa na harakati hiyo ya Kiislamu.

Akizungumza na kanali ya televisheni ya Al-Mayadin ya nchini Lebanon, Ismail Haniyeh sambamba na kutupilia mbali kufanya uhusiano wowote wa kidiplomasia na Marekani, kwa mara nyingine amesisitizia kufungwa njia zote za udhibiti wa Washington kwa eneo hili. Haniyeh amesema kuwa umoja wa Wapalestina kwa ajili ya kukabiliana na mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne ni wenye umuhimu sana na kubainisha kuwa, juhudi za aina yoyote kwa ajili ya kuibua tofauti kati ya harakati ya Hamas na Jihadul-Islami, zimefeli kwa kuwa muqawama wa Ukanda wa Gaza haukubali kushindwa.

Akizungumzia safari yake ya hivi karibuni mjini Moscow, Russia Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS amesema kuwa ili kuweza kufikia mtazamo mmoja, harakati hiyo iliwasilisha machaguo yake manne kwa Russia ambayo ni uchaguzi mkuu, kufanyika bunge la kitaifa la Palestina nje ya mji wa Ramallah, kufanyika kwa kongamano kuu la kitaifa la Palestina mjini Cairo Misri na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina.

Jumatatu iliyopita Ismail Haniyeh akiwa mjini Moscow alikutana na Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na kujadiliana naye mipango ya kisiasa ya ukombozi wa Palestina na njia za utatuzi wa kudumu na amani katika eneo la Asia Magharibi.

Jumanne ya tarehe 28 Januari, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.

Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. Mpango huo unaendelea kulaani kimataifa n ahata ndani ya Marekani kwenyewe.

3883082

captcha