IQNA

Ayatullah Sistani: Wafanyakazi wa sekta ya afya wanaofariki kutokana na corona ni mashahidi

21:22 - March 17, 2020
Habari ID: 3472576
TEHRAN (IQNA)- Mwanazuoni wa ngazi za juu kabisa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatullah Sayyid Ali al-Sistani amesema madaktari na wauguzi ambao wanawatibu wagonjwa wa COVID-19 au kirusi cha corona na kisha wanapoteza maisha baada ya kuambukizwa kirusi hicho wakiwa kazini watahesabiwa kuwa ni mashahidi.

Akijibu swali  la kidini (Istifta),  Ayatullah Sistani ameongeza kuwa, kuwatibu wanaougua corona ni Wajib Kifai.
Wajib Kifai hapa ni kwamba, ni wajibu wa kila Mwislamu, lakini mara tu jukumu hilo linapotekelezwa kwa usahihi na Mwislamu yeyote, hukoma kwa wajibu kwa Waislamu wengineo; lakini kama akikosekana mtu wa kumsaidia mgonjwa huyo, kila Mwislamu (atakayekuwepo hapo) atapata dhambi.
Ayatullah Sistani ameongeza kuwa, maafisa husika wanapaswa kuwapa wafanyakazi wa sekta ya afya vifaa vyote wanavyohitaji na kuwalinda wasiambukizwe. Aidha amesema ni jambo lisilokubalika kuwepo uzembe katika jambo hili.
Wiki iliyopita pia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliafiki pendekezo kuwa, wafanyakazi wa sekta ya afya wanaofariki wakiwa katika mstari wa mbele wa kupambana na ugonjwa wa COVID-19 wahesabiwe kuwa ni mashahidi.
captcha