IQNA

Majeshi ya Yemen yadhibiti kambi ya kijeshi ya muungano wa Saudia mkoani Ma’rib

9:42 - March 18, 2020
Habari ID: 3472577
TEHRAN (IQNA) - Majeshi ya Yemen yakishirikiana na kamati za Harakati ya Wananchi ya Answarullah yamefanikiwa kudhibiti eneo la Kufal, ambapo kuna kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya muungano vamizi wa Saudi Arabia katika mkoa wa Ma'rib, katikati mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa duru za habari nchini Yemen, kambi kubwa ya Kufal, iliyokuwa ikidhibitiwa na wanagambo watiifu kuwa  rais waliyejiuzulua nchini humo, Abdrabbuh Mansur Hadi, imetwaliwa na kwamba sababu ya jambo hilo ni kujiri operesheni kali za jeshi la Yemen na kamati za wananchi kutokea pande tatu kuelekea mkoa wa Ma'rib.

Kadhalika Majid Al-Sha'bi, Mkuu wa Idara ya Habari  katika mji wa Ad Dali amekiri kuwa, baada ya Harakati ya Wananchi ya Answarullah kudhibiti ngome zote za mkoa wa Al Jowf na Ma'rib, imetwaa silaha za kisasa za muungano vamizi wa Saudia ambazo zinaweza kutosha kwa vita vya miaka mitano.

Baadhi ya duru za habari zimearifu kwamba kuna mgogoro mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa kati ya wanamgambo wenye mafungamano na Imarati na wale wenye mafungamano na Saudia katika mkoa wa Aden, kusini mwa Yemen.

Kwa mujibu wa duru za eneo hilo, askari wa Baraza la Mpito la kusini mwa Yemen wenye mafungamano na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wameanzisha vituo vya kijeshi katika malango na barabara za mji wa Aden, na kuudhibiti mji huo sambamba na kuendesha operesheni za upekuzi katika mji huo.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 16,000 wanaripotiwa kupoteza maisha katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.

3470946

captcha