IQNA

Salamu za Nowruz (Nairuzi) za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

17:57 - March 20, 2020
Habari ID: 3472585
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za kheri na fanaka kwa munasaba wa kuwadia siku kuu ya Nowruz (Nairuzi) ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia na wakati huo huo akatuma salamu za rambi rambi kutokana na kupoteza maisha idadi kubwa ya watu kutokana na ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Katika salamu zake hizo kwa munasaba wa Nowruz, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea matumaini yake kuwa, pamoja na kuwepo majonzi yaliyoenea kote kutokana na corona, siku kuu ya Nowruz itaweza kuwaletea wanaadamu furaha.

Katika ujumbe wake huo  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Mwaka huu, sherehe za Nowruz zinaanza wakati wa majonzi na masikitiko. Ugonjwa wa COVID-19 umeenea duniani kote ikiwa ni pamoja na maeneo yanayoadhimisha sherehe hii kongwe."

Gutteres amesema, 'Kila mwaka huwa tunaadhimisha Nowruz kama siku ya mwanzo mpya, wakati tunapoingia katika mwaka mpya kwa matumaini na furaha. Sisi huadhimisha kuhuishwa tena mazingira na pia tunaadhimisha siku ya kwanza ya msimu wa machipuo."

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, watu wasiopungua 255,000 wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19 kote duniani na miongoni mwao zaidi ya 10,000 wameaga dunia.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz au Nairuzi. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania.

Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin sawa na 21 Machi kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

3886524

captcha