IQNA

Mabaath ya Mtume Muhammad SAW na Malengo Yake

17:47 - March 22, 2020
Habari ID: 3472593
TEHRAN (IQNA) - Leo ni tarehe 27 Rajab kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria na katika siku kama ya leo miaka 1454 iliyopita, Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad Mustafa SAW alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu.

Mabaath ya Mtume Muhammad SAW na Malengo Yake

Katika siku za kukaribia tarehe 27 Rajab Mohammad SAW alikuwa akienda katika pango la Hiraa na katika baadhi ya nyakati alikuwa akikaa siku kadhaa katikaeneo hilo. Alikuwa akimfahamisha mke wake  mtiifu Khadija kuwa: ‘Wewe pia wafahamu mahaba na mafungamano yangu.Katika siku hizi nina hisia ya ajabu ya kupenda kumkumbuka Mola  muumba, moyo wangu hautaki chochote isipokuwa hilo.’

Usiku uliojaa siri

Hatimaye usiku uliojaa  siri uliwadia.Mwezi uliangazia nuru yake katika eneo la kusini lamlima.  Kulikuwa na kimya mutlaki na cha ajabu katika kila sehemu. Ilikuwa ni kana kwamba mbingu na ardhi ilikuwa inasibiri tukio adhimu.

Mohammad SAW alikuwa akikesha katika aghalabu ya nyusiku. Hakuna sauti iliyokuwa ikisikika katika milima usiku huo. Kimya na utulivu wa usiku huo ulikuwa na maana maalumu. Katika lahadha hiyo iliyojaa siri kubwa, nuru ya kutoka mbinguni iliangazia upeo wa Mtume Muhammad SAW. Alihisi mtikisiko katika mwili na roho yake. Katika lahadha hiyo, ghafla kiumbe adhimu alijitokeza mbele ya macho ya Mohammad. Alikuwa kiumbe mwenye adhama na utukifu. Kila upeo alioangalia katika mbingu, Mohammad alimuona kiumbe huyo aliyejaa nuru. Alikuwa ni Malaika wa Wahyi, Jibril. Hapo Jibril alimkaribia Mohammad na kunena ifuatavyo.

Soma kwa jina la Mola wako

Ewe Mohammad Soma. Mohammad alitazama kwa makini.  Aliona maandishi mbele ya uso wake. Kwa mara nyingine sauti ikaja  na kusema, ‘Soma kwa jina la Mola wako. Kwa sauti ya iliyotikisika, Mohammad aliuliza, Je nisome nini? Sina ujuzi wa kusoma.Hapo malaika alisema:

Soma kwa jina la Mola Wako aliyeumba. Amemumba mtu kwa pande la damu. Soma! Na Mola Wako ni Karimu Zaidi!  Ambaye amefundisha kwa kalamu. Amemfundisha mtu aliyokuwa hayajui. Surat Al-`Alaq (1-5)

Mohammad, ambaye  uwepo wake wote  ulikuwa unabubujika kwa mahaba ya mbinguni, alianza kusoma na Malaika Jibril.

Kwa mara nyingine Mohammad alisikia sauti ikimwambia:  ‘Ewe Mohammad wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu’  Hii  haikuwa ndoto bali, lilikuwa ni tukio la kweli.  Naam, alikuwa katika irada ya Mwenyezi Mungu na kupata taufiki ya kuwa mja ambaye Mwenyezi Mungu alizungumza naye. Mwenyezi Mungu SWT alimteua Mohammad SAW  miongoni mwa viumbe wengine na alimtambua kamamwenye ustahikiwa kupokea Wahyi.Mohammad SAW ambaye daima alikuwa akiwaza na kutafakari kuhusu namna kuwaokoa watu kutoka katika upotofu, hivi sasa alikuwa na jukumu adhimu.

Kuteuliwa kwa Mtume

Alipata hisia ajibu katika mwili na roho yake. Alihisi joto kali sana. Mabega yake  yalitikisika kwa msisimko aliokuwa nao. Alitaka kusimama kutoka sehemu aliyokuwpo. Hatahivyo alihisi kutokuwa na uwezo. Hapo alianguka chini kwa paji la uso bila kuhiyari alianza kutokwa na machozi. Katika usiku huo uliojaa msismuko yaani mkesha au usiku wa kuamkia tarehe 27 Rajab, Mohammad SAW aliteuliwa kuwa Mtume. Mitume wote wa Mwenyezi Mungu wametumwa naye ili waweze kumuongoza mwanaadamu kutoka katika kiza cha ujahili na shaka hadi katika nuru ya elimu na maarifa. Tab’an kila moja wa mitume hao alitumia mbinu maalumu za kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kutegemea hali katika zama alizoishi.

Suala muhimu na lenye taathira katika kuenea mafundisho aliyokuja nayo Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW ni shakhsia yake muhimu pamoja na sifa za kipekee za ujumbe wake.

Yaliyomo katika Aya za Qur’ani Tukufu ni mjumuiko wa maarifa yenye mafunzo muhimu na yenye thamani. Maarifa ya Qur’ani Tukufu yanaenda sambamba na akili na pia uondoa utata ulio katika akili za watu. Sifa hizo za kipekee za Qur’ani Tukufu ndio chanzo cha wenye kutafuta haki kuvitiwa na kuamua kufuata Uislamu.

Mtume Muhammad SAW,  alibainisa na kufafanua kuhusu ujumbe wake kwa msingi wa mantiki, dalili za wazi na kwa ufasaha wa hali ya juu.  Alifafanua kikamilifu na kwa uwazi kuhusu kumuabudu Mwenyezi Mungu moja. Huyu ni Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi na yaliyomo.

Mtume SAW daima alikumbusha kuhusu ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu katika maumbile ya dunia na hivyo kupelekea  watu wamzingatia Mola Muumba. Alibainisha kuwa dunia imeumbwa kwa msingi wa nidhamu maalumu na erevu.

UjumBe wa Mtume Mtukufu SAW

Katika ujumbe wa Mtukufu Mtume SAW alibainisha ufahamu kuhusu nukta kama vile kutafuta ukweli, kusimamia uadilifu na kuwepo uhusiano mzuri na salama baina ya wanaadamu. Mafundisho aliyobainisha Mtume SAW ni mafunzo yaliyoenda sawia na maumbile asilia na fitra ya mwanadamu. Watu waliokuwa na masaibu katika zama hizo za kudhihiri Uislamu waliweza kupata uhai mpya kutokana na mafundisho ya Mtume Muhammad SAW ambaye aliwapa bishara njema za maisha mazuri na yenye saada. Ni wazi kuwa iwapo maarifa ya Uislamu haukuwa na sifa za kipekee basi dini hii haingeweza kuenea miongoni mwa walimwengu. Ujumbe wa Mtume SAW uliwezi kupenya na kukita mizizi katika nyoyo za watu walioukubali na kuufuata.

Kati ya nukta muhimu katika itikadi ya Kiislamu na ambayo pia ilikuwa moja ya malengo ya juu ya Mtume SAW ni elimu na malezi.  Mtume  Muhammad SAW alifuatilia na kusisitiza sana kuhusu kueneza elimu na maarifa sambamba na malezi bora ya kiroho.

 

Yeye Ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma

Qur’ani Tukufu katika aya pili ya Surat Jumua malengo ya Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW yameashiriwa ifuatavyo: Yeye Ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, aliyetokana na wao, awasomee Aya Zake, na awatakase, Na awafunze Kitabu na hikima, Japokuwa hapo kabla walikuwa katika upotofu uliodhahiri.

Kwa msingi huo, Mtume Muhammad SAW alikuwa na jukumu la kusoma aya hizo za Mwenyezi Mungu ambazo huinua hadhi ya mwanaadamu ili kutakasa nafsi za watu na kuwaondoa katika dimbwi la upotofu wa shirki na itikadi batili  ili wawezi kuwa ni wenye akhlaqi au maadilibora. Katika kubainisha lengo hilo Mtume Mtukufu SAW alisema: “Hakika mimisikutumwa ila kukamilisha maadili mema”

Kwa hivyo kati ya malengo muhimu ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho, SAW yametajwa katika Qurani Tukufu kuwa ni pamoja na kutakasa nafsi na kuwalea wanaadamu ili waweze kustawi na kufikia daraka lajuu la mwanadamu. Ni katika kivuli hiki ndio uhusiano wa mwanadamu na Muumba hurekebishwa katika jamii ya Kiislamu.

Mtume Muhammad SAW si tu katika maneno bali pia katika vitendo alikuwa  kigezo bora zaidi kwa manaadamu katika upeo wa maadili mema. Mtukufu huyo aliwaongoza watu na kuwa mfano wa kuigwa na wengine katika utekelezaji mafundisho na amali za Kiislamu. Hulka njema na tabia iliyojaa ukarimu ya Mtukufu huyo miongoni mwa watu ni nukta ambazo zilikuwa na mvuto wa kipekee.

Akhlaqi bora

Taathira hii ya kipekee ya akhaqi bora za Mtume SAW ndio nukta ambayo ilipelekkea Waarabu wa zama za Ujahiliya au ujinga wajikusanya kando kando ya mtukufu huyo ili  waweze kupata mafundisho ya Muongozo wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mtukufu huyo.

Katika zama za Risala ya Mtume  wa Uislamu SAW , kipindi kigumu zaidi kilikuwa  ni wakati wa jitihada za kubadilisha na kuondoa itikadi potofu za Waarabu na ushirikina. Aghalabu walikuwa ni watu wenye taasubu sana. Katika amzingira hayo magumu, ili kupata mafanikio katika kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu SWT, Mtume Mtukufu SAW alitegemea nukta muhimu sana.

Mtukufu huyo aliheshimu shakhsia yamwanaadamu hata ya watu waliokuwa na taasubu. Alijitahidi kuhakikisha kuwa kunapatikana mazingira tulivu na yasiyo na utata ili aweze kueneza ujumbe aliokuwa nao.  Mtume SAW hata alijiepusha kuwadhalilisha watu majahili au wajinga na iwapo alilazimika kuingia katika mdahala hakuwa akiwakejeli na alikuwa akitafuta fursa muafaka ya kuendeleza mazungumzo nao. Katika kufikisha ujumbe wa haki, Mtume SAW aghalabu alikuwa akianzia katika nukta ambayo inakubaliwa na upande wa pili. Alitumia sana mbinu hii katika midahalo yake ni Ahul Kitab.

Mtume Muhammad SAW alikuwa akizingatia kwa kina uwezo wa ufahamu wa kila mtu na kasha hapo alibainisha ujumbe wake.

Mtume Mtukufu SAW alikuwa na uhusiano na watu wa matabaka mbali mbali makundi ya kila umri. Kwa hivo Mtukufu huyo ujumbe wa mtukufu huyo uliwalenga wazee, vijana, wanaume, wanawake, masikini, tajiri, wenye  elimu na wasiokuwa na elimu.

Uzingatiaji Sira

Wakati Mtume SAW alipokuwa akiwahutubu Ahlul Kitab, alikuwa akianza na nukta za pamoja baina ya dini zao na Uislamu. Baadhi ya wakati tabasamu tamu na mtazamo   wa kina kwa jicho la Mtukufu huyo ni jambo ambalo lilivutia nyoyo na kuwa na ushawisho kamili kwa hadhirina ambao walipata muongozo kupitia mafundisho yake ya haki na yenye kutoa muongozo.

Mtume Mtukufu SAW daima alijitahidi kuwafikishia wanaadamu ujumbe wa haki katika kivuli cha  kumcha Mungu Moja Muumba wa Mbingu na Ardhi. Ni kwa msingi huo ndio moja kati ya nara na kauli mbiu aliyotumia ni: ‘Sema Hakuna mungu Apasaye Kuabdiliwa ila Mungu Moja ili ufanikiwe’.

Hivi sasa katika siku hizi zilizojaa masaibu tunashuhudia Waislamu  na wasio kuwa Waislamu wasio na hatia wakiuawa mikononi mwa watu sawa na waliokuwa katika zama za ujahiliaya.

Kumbukumbu ya kubaathiwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Mohammad Al Mustafa SAW ni fursa nzuri ya kuzingatia kwa kina na kufuata mafundisho yenye kuleta saada ya Uislamu na Sira tukufu ya Mtukufu huyo.

Kwa hakika Maarifa ya Qur’ani Tukufu, Sira ya Mtume SAW na Ahul Bayt wake ni taa na nuru za kuwaondoa watu walio katika kiza za ujahili au ujinga za zama hizi.

 

captcha