IQNA

Jumamosi 25 Aprili inatazamiwa kuwa Ramadhani Mosi nchini Iran

0:23 - April 23, 2020
Habari ID: 3472695
TEHRAN (IQNA) – Mwanachama wa Kamati ya Hilali ya Mwezi nchini Iran amesema hilali ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani haitazamiwi kuonekana Alhamisi Aprili 23.

Katika mahojiano na Shirika la Habari la IQNA, Hujjatul Islam Ali Ridha Mowahidnejad amesema wataalamu wanaamini kuwa hakutakuwa na uwezekano wa hilali ya mwezi kuonekana Alhamisi hii na kwa msingi huo Ijumaa haitakuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Ameongeza kuwa, uwezekano mkubwa ni kuwa, Ijumaa 24 Aprili itasadifiana na tarehe 30 Shaaban na hivyo siku inayofuata, yaani Jumamosi Aprili 25 itakuwa tarehe 1 Ramadhani mwaka 1441 Hijria Qamaria.

Pamoja na hayo, Hujjatul Islam Mowahidnejad amesema timu za kuitazama hilali zitatumwa kote Iran Alhamisi.

Akiashiria suala la hilali ya mwezi katika nchi jirani na Iran amesema: “Katika baadhi ya nchi jirani, kama ilivyo ada yao ambayo tumeishuhudia katika miaka iliyopita, kuna uwezekano mkubwa kuwa Ijumaa kwao itakuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.”

Amesema nchi hizo hutegemea watu wasio wataalamu na wenye uzoefu duni kutekeleza zoezi la kufuatilia hilali na hivyo huchanganyikiwa katika kuuona mwezi na hufikisha ripoti kwa idara zao za kidini ambazo nazo hutangaza kuanza au kumalizika mwezi kwa kutegemea ripoti hizo.

Katika hali ambayo baadhi ya wanazuoni wanategemea mahesabu ya nujumu au ‘mwezi wa kimataifa’ kuainisha kuanza miezi ya Hijria Qamaria, wanazuoni katika nchi nyingi za Kiislamu, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huwa na kamati maalumu kutazama hilali kwa lengo la kuthibitisha kuanza au kumalizika miezi, ukiwemo Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

3471229

captcha