IQNA

Uturuki yasema itaulinda mji wa Tripoli Libya usitekwe na Haftar

19:18 - April 29, 2020
Habari ID: 3472715
TEHRAN (IQNA)- Uturuki imemtuhumu jenerali muasi Khalifa Haftar wa Libya kuwa analenga ‘kuibua udikteta wa kijeshi’ na hivyo imeapa kuulinda mji wa Tripoli.

Jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi la wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) siku ya Jumatatu alijitangaza mtawala mpya wa nchi hiyo katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni na kuyafuta makubaliano ya mwaka 2015 yanayojulikana kama "Makubaliano ya Skhirat". Alisema ataongoza serikali ya mpito hadi wakati wa kufanyika uchaguzi.

Kufuatia dai hilo la Haftar, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imetoa taarifa na kusema: “Kwa tangazo hilo, Haftar kwa mara nyingine amethibitisha kuwa hataki suluhisho la kisiasa kwa mgogoro wa Libya, na haungu jitihada za kimataifa kuhusu nukta hiyo, lengo lake kuu likiwa ni kuibua udikteta wa kijeshi nchini humo.”

Wakati huo huo, Stephanie Williams, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametangaza kuunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Fayez al-Sarraj  na kuongeza kuwa: "Mabadiliko yoyote ya kisiasia nchini humo yanapaswa kufanyika kwa njia ya demokrasia.

Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imesema tangazo la Haftar ni mapinduzi ya serikali na ni njia ya kujaribu kufunika kushindwa kwake kijeshi. Katika wiki za hivi karibuni, wanamgambo wanaofungamana na Haftar wameshindwa vibaya katika mapigano na wanajeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya.

Aprili mwaka jana, Haftar alianzisha mapigano kwa lengo la  kuukalia kwa mabavu mji wa Tripoli na kuitimua serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya. Alianzisha mapigano wakati ambao mchakato mpya wa mazungumzo ya amani ya Libya ulikuwa nao pia ndio unaanza. Nukta hii inaashiria kuwa yeye na waitifaki wake hawakuwa wanataka mabadilishano ya madaraka kwa njia ya kisiasa.

Jenerali muasi Haftar anapata uungaji mkono wa nchi kama vile Saudi Arabia, Imarati (UAE), Misri na baadhi ya nchi za Ulaya na hivyo ni kwa idhini ya waungaji mkono hao ndio amevuruga mchakato wa kisiasa Libya. Wakati alipoanzisha hujuma dhidi ya Tripoli, Haftar alidhani kuwa angepata ushindi wa haraka na hivyo kuchukua madaraka lakini alikumbana na jibu kali la wanajeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaba ambayo inapata uungaji mkono wa kijeshi wa Uturuki.

3471311

captcha