IQNA

Iran yalaani vikali vikwazo vya Marekani vinavyozuia ushirikiano wa kimataifa

23:30 - May 31, 2020
Habari ID: 3472821
TEHRAN (IQNA) - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hatua mpya zilizochukuliwa na Marekani za kuuwekea vikwazo ushirikiano wa kimataifa wa nyuklia baina ya Iran na pande nyingine na kusema kuwa kitendo hicho kinavunja waziwazi azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mapema jana, Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba: "Ninahitimisha misamaha ya vikwazo ya miradi ya nyuklia inayohusiana na JCPOA nchini Iran na hilo litaanza kutekelezwa baada ya siku 60.

Leo Jumamosi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Sayyid Abbas Mousavi amelaani hatua hizo mpya za chuki na za kiuadui za Marekani dhidi ya taifa la Kiislamu la Iran na kusema, kitendo hicho kinadharau haki ya kimsingi kabisa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kinautia kwenye matatizo mfumo jumla wa kimataifa.

Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatilia kwa karibu athari za kiufundi na kisiasa za hatua hiyo na iwapo zitakuwa na mathari mbaya kwa haki ya nyuklia ya Iran kwa mujibu wa hati ya kimataifa na vipengee vya mapatano ya JCPOA, basi Tehran itaamua ni namna gani itachukuwa hatua za kisheria za kujibu uadui huo wa Marekani.

Ikumbukwe kuwa tarehe 8 Mei 2018, Trump aliitoa kijeuri Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yenye baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Viongozi waliopita wa Marekani walikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha makubaliano hayo, lakini Trump ametia ulimi puani kwa kuitoa Washington nje ya mapatano hayo na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano ya JCPOA.

3901980

captcha