IQNA

Imam Khomeini alifungua ukurasa mpya katika kumfanya mwanadamu amkurubie Mwenyezi Mungu

15:58 - June 03, 2020
Habari ID: 3472831
TEHRAN (IQNA) - Tarehe 14 Khordad sawa na tarehe 3 Juni, kulitangazwa habari ya huzini ya kuaga duniani Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tukiuo hilo la huzuni si tu kwamba lilihuzunisha taifa la Iran pekee bali lilihuzunisha na kuwasababishia majonzi makubwa wapenda haki na uhuru pamoja na wale wote wanaopigana dhidi ya dhulma duniani.
Mara tu baada ya kusikia habari hiyo, Wairani wote walimiminika mitaani huku wakiwa wanabubujikwa machozi na kujipiga vifua kwa huzuni kubwa waliyopata kutokana na kumpoteza kiongozi wao huyo mpendwa. Mapenzi makubwa waliyokuwanayo kwa kiongozi wao huyo yalipelekea kufanyika mazishi makubwa zaidi kuwahi kuonekana katika historia ya zama hizi. Katika sehemu ya mazishi hayo, mwili mtakatifu wa Imam Khomeini (MA) uliwekwa kwenye jeneza la kioo ambapo watu kutoka pembe zote za nchi walifika mjini Tehran kwa ajili ya kupata fursa ya kumuaga Imam wao huyo mpendwa. Hali hiyo ilidhihirisha mandhari ya kupendeza ya jinsi taifa la Iran lilivyokuwa na upendo mkubwa kwa kiongozi wao huyo, Imam Khomeini (MA).
 
Mazishi makubwa
 
Mazishi hayo ya Imam Khomeini yalitangazwa na kuakisiwa na magazeti, redio na televisheni mbalimbali za humu nchini, kieneo na kimataifa na kwa muda fulani yaliendelea kuwa katika kilelel cha habari zilizotangazwa na vyombo hivyo vya habari. Kuhusu suala hilo shirika la habari la France Press lilisema: 'Licha ya kuwa siku nzima imepita tokea kuzikwa Imam Khomeini, lakini bado maelfu ya watu wamekusanyika kwenye kaburi hilo katika makuburi ya Beheshti Zahra, wanaomba dua na kujipiga vichwa na vifua ambapo wote wamauamua kulifanya eneo hilo kuwa moja ya maeneo matakatifu katika ulimwengu wa Kiislamu.' Ni wazi kuwa maombolezo hayo ya hamasa yaliendelea kwa muda wa siku nyingine nyingi baada ya maziko hayo.
Gazeti la Marekani la International Herald Tribune liliandika hivi katika moja ya matoleo yake kumuhusu Imam Khomeini (MA): 'Ayatullah Khomeini alikuwa mwanamapinduzi asiyechoka na ambaye hadi kufariki kwake alikuwa meshikamana vilivyo na malengo yake ya kuasisi jamii na serikali ya Kiislamu nchini Iran. Hakusita hata kidogo kufuatilia kile alichotaka kwa ajili ya nchi yake kongwe. Aliufanya kuwa wajibu wake kufuta na kusafisha nchini Iran ufisadi na kila alichokiona kuwa ni ufuska wa nchi za Magharibi na kuirejeshea jamii mafundisho sahihi na halisi ya Uislamu.'
 
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
 
Kwa uungaji mkono mkubwa wa wananchi, hatimaye Imam Khomeini aliyafikisha kwenye ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979, jambo lililosambaratisha kabisa mahesabu ya ulimwengu wa Mgharibi. Alianzisha harakati yake ya kimapinduzi kwa lengo la  kuhuisha fikra za kisiasa za Uislamu nchini. Moja ya tofauti za kisiasa za mwamko na harakati ya Imam Khomeini ikilinganishwa na harakati nyingine zilizodhihiri ulimwenguni katika karne za hivi karibuni, ni sifa maalumu na uwezo mkubwa wa dini tukufu ya Uislamu kama ilivyobainishwa na Mtume Muhammad mwenyewe (saw). Katika ulimwengu ambao mwanadamu alikuwa amefanya matamanio yake kuwa lengo lake kuu na wakati huohuo kubana mafundisho ya dini katika mipaka ya kuta za misikiti tu na hivyo kuyafanya kutokuwa na nafasi yoyote katika maisha yake ya kila siku, Mapinduzi hayo ya Imam Khomeini (MA) yaliyotokana na mafundisho halisi ya Uislamu yalidhihiri na kuwa na taathira kubwa ulimwenguni. Imam ambaye alikuwa mwanazuoni, arif, aliyemtambua vyema Muumba wake, mwenye takwa, mwenye mwamko na mtazamo wa kina wa kisiasa na kijamii, aliweza kudhihirisha na kutekeleza vyema mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu na hivyo kufanikiwa kufungamanisha vizuri maisha ya kimaada na kimaanawi ya mwanadamu.
Harakati ya Imam Khomeini (MA) ilitokana na mabumbile safi ya mwanadamu, maumbile ambayo hayakinaishwi tu na mahitaji ya kimaada na ladha za kidunia ambazo hupita na kumalizika haraka bali hiutajia mahitaji mengine muhimu ambayo ni ya kiroho na kimaanawi. Imam Khomeini (MA) aliingia uwanjani ili kuadhamini na kukidhi mahitaji hayo muhimu ya mwanadamu na wakati huohuo kuwadhihirishia walimwengu utajiri mkubwa wa dini tukufu ya Uislamu iliyoletwa na Mtume Muhammad (saw), dini ambayo haibani thamani za kimaanawi katika  mipaka ya kuta za makanisa, mahekalu na misikiti bali huzisambaza katika pande zote za maisha ya mwanadamu ili kumfanya aweze kufikia malengo yake ya juu maishani. Kwa kusikiliza hotuba zake zenye thamani ni kana kwamba watu walikuwa wakimsikia Imam akiwaambia: 'Rudini kwenye mafundisho ya Mwenyezi Mungu na msikubali dhulma, ufisadi na uonevu na simameni mpambane kwa ajili ya kuhuisha mafundisho ya mbinguni ambayo yameletwa na Uislamu.'
 
Misimamo inayofaa
 
Kwa kuchukua misimamo ya kisiasa inayofaa na kwa wakati, kutoa hotuba za hamasa na zenye taathira kubwa pamoja na taarifa zilizoratibiwa vizuri, Imam alithibitisha wazi kwamba alikuwa kiongozi mwenye mwamko na busara kubwa. Kwa kutambua vyema mazingira ya kisiasa na kijamii na vilevile mahitaji na matatizo ya kisiasa, kiutamaduni na kijamii ya watu, Imam (MA) alileta mabadiliko makubwa na hivyo kuweza kuhuisha moyo mpya nchini Iran na hatimaye kufanikiwa kuiweka nchi katika njia sahihi ya kuhuishwa thamani za kidini na kiutamaduni.
 
Profesa Lancer wa Austria anasema kuhusu Imam Khomeini, Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran: 'Alifungua ukurasa mpya katika kumfanya mwanadamu amkurubie Mwenyezi Mungu na kwa uungaji mkono wa wananchi, akafanikiwa kuyaletea ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalikuwa na taathira kubwa katika historia ya karne ya 20.'
 
Lengo kuu la mapambano na harakati ya Imam Khomeini (MA) dhidi ya dhulma, ufisadi na utawala wa Shah wa Iran halikuwa jingine bali lilikuwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuhuisha mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. Yeye mwenyewe alifuata kikamilifu mafuindisho hayo katika maisha yake binafsi na ya kifamilia. Mfano wa hilo ni kwamba alikuwa na maisha mepesi na ya kawaida kabisa yaliyokuwa mbali na sifa za kujifakharisha. Hakuwa akitumia vifaa na suhula zaidi ya alivyohitaji maishani. Chakula, mavazi na makazi yake yalikuwa ya chini kuliko ya watu wengi wa kawaida na akisisitiza sana juu ya kuzingatiwa zuhdi na kukinai maishani. Pamoja na hayo hakuwa mtu wa kujitenga na watu na daima alikuwa akifuatilia masuala ya jamii yake na ya nchi nyingine. Daima alikuwa akifikiria na kuwajali wanyonge, masikini na waliodhulumiwa na kuhuzunishwa sana na matatizo waliyokuwa wakiyapitia waliyosababishiwa na mustakbirina na madhalimu wa dunia. Profeda Monty wa Ufaransa anazungumzia maisha hayo mepesi na ya kawaida kabisa ya Imam Khomeini (MA) alipokuwa akiishi katika eneo la Nofel Loshato katika viunga vya mji wa Paris Ufaransa kwa kusema: 'Nilishangazwa sana na maisha ya kawaida ya Imam kuliko jambo jingine lolote. Akiwa Paris, Imam alikuwa akiishi kwenye nyumba ndogo kabisa ambayo haikuwa na zaidi ya vyumba viwili. Chumba kimoja kilikuwa cha malazi yake ni cha pili kilikuwa cha kazi zake na kuwalaki wageni. Hakuna kitu chochote chenye thamani kilichoonekana kwenye maisha yake.'
 
Aliongoza nyoyo za watu
 
Katika kipindi cha uongozi wake, Imam Khomeini (MA) ambaye alikuwa mwanafalsafa, mwanasiasa na mtu aliyemwogopa sana Mwenyezi Mungu si tu kwamba alikuwa mwanasiasa bali pia alikuwa arif mkubwa ambaye alikuwa akiziongoza nyoyo za watu.
 
Bila shaka watu kama hawa hupatikana tu kupitia mafundisho ya Qur'ani na Uislamu. Watukufu kama hawa hufikia daraja hiyo ya juu kimaanawi kupitia juhudi kubwa za utakasaji wa nafsi na msaada mkubwa wanaoupata kutoka kwa Mwenyzi Mungu. Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mbaye mwenyewqe ni mwanafunzi wa chuo na fikra ya Imam Khomeini (MA) anasema kuhusiana na shakhsia huyu mkubwa: 'Hakuna tukio lolote ambalo lingeweza kushinda na kumvunja nguvu Imam na kumfanya alidhalilikie. Katika matukio yote machungu na magumu ambayo yalitokea katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake, Imam alitokea kuwa mshindi wa matukio hayo yote, hakuna tukio lolote kati ya hayo, iwe ni vita vya miaka minane, mashambulio ya Marekani, majaribio ya mapinduzi, mauaji ya kigaidi ya kutisha, vikwazo vya uchumi na mambo mengine makubwa tofauti na ya kushtua yaliyotekelezwa na maadui, yote hayo hayakuweza kudhoofisha wala kumshinda mtukufu huyu. Alikuwa ni mwenye nguvu na mkubwa zaidi kuyashinda matukio hayo yote.'
 
Aliheshimu wananchi
 
Imam Khomeini (MA) aliwapenda sana watu na kuheshimu matakwa yao. Aliheshimu, kuthamini na kuyapa umuhimu mkubwa maoni na matakwa yao. Alikuwa mpole kwa watu na kujiona kuwa mtumishi wao. Alikuwa akiwasisitizia viongozi wawahudumie wananchi na kulinda heshima zao. Alikuwa akisema: 'Watu wanapomkataa mhudumu fulani anapasa kuondoka.' Alikuwa akiwasisitizia viongozi kuwahudumia kwa dhati wananchi na kuitowapuuza. Akisema: 'Wahudumieni watu hawa waliodhulumiwa, watu ambao wamekufikisheni hapa mlipo......Tunapasa kuwahudumia hawa, kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake.'
 
Kutokana na majukumu yake ya kibinadamu na Kiislamu, Imam Khomeini (MA) pia aliupa umuhimu mkubwa ukombozi wa mataifa mengine ya duniani yaliyokuwa yakidhulumiwa kwa njia tofauti. Anasema katika moja ya hotuba zake: Ninatumai kwamba harakati na  mapinduzi haya yataishia katika kudhihiri kwa Imam wa Zama (af) na kuinufaisha dunia na wanyonge wote. Tunataraji kwamba yataweza kuwaokoa wanyonge na kufika katika pembe zote za dunia na kuwawezesha wote kufuata njia mliyoifuata nyinyi ya kuwashinda maadui wa Uislamu na wa taifa, ili wanyonge pia waweze kuwashinda mustakbireen.'
captcha