IQNA

Kuwait kuruhusu Swala za Ijumaa baada ya miezi minne

19:49 - July 15, 2020
Habari ID: 3472965
TEHRAN (IQNA) – Kuwait imesema inapanga kuruhusu tena Swala za Ijumaa wiki hii, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Taarifa zinasema Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu Kuwait imesema imeamua kuondoa marufuku ya miezi minne ya Swala baada ya hatua imara kuchukuliwa kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19. Hatahivyo, maafisa wa afya wameonya kuwa misikiti itafungwa tena iwapo waumini hawatazingatia masharti ya afya yaliyowekwa.

Zaidi ya misikiti 1,000 inatazamiwa kufunguliwa kote nchini Kuwait. Kati ya masharti yatakayofuatwa ni kuwa misikiti itafunguliwa dakika 30 kabla ya adhana na kufungwa dakika 15 baada ya Swala. Aidha hotuba na swala haitazidi dakika 15 na waumini wote wanatakiwa kuvaa barakoa wakati wote wakiwa msikitini. Halikadhalika waumini wametakiwa wazingatie sheria ya kutokaribiana wakiwa ndani ya msikiti na kila moja aswali sehemu maalumu iliyowekwa alama.  Aidha vyoo vya  misikiti havitafunguliwa na waumini wametakiwa washike udhu nyumbani kabla ya kufika msikitini.

Sheria zingine ambazo zimetajwa ni kumtaka kila muumini afike msikitini akiwa na mkeka wake binafsi wa kuswalia na pia kujiepusha kupeana mkono au kugusana ndani ya msikiti. Halikadhalika watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 hawataruhusiwa kuingia msikitini na watu wenye dalili za COVID-19 nao pia wameombwa wasifike msikitini.   

3472022/

captcha