IQNA

Utawala wa Israel waendelea kushinikizwa kuhusu Palestina

13:41 - July 16, 2020
Habari ID: 3472967
TEHRAN (IQNA) - Utawala haramu wa Kizayuni umekusudia kunyakua asilimia 30 zaidi ya ardhi za Palestina za Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ilizozivamia na kuanza kuzikalia kwa mabavu mwaka 1967 na kuziunganisha na ardhi zingine ilizozipa jina la Israel, ukiwa ni muendelezo wa malengo yake ya muda mrefu ya kuikalia kwa mabavu Palestina yote.

Hatua hiyo haramu na inayohalifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imepingwa duniani kote hata na nchi za Ulaya.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, siku ya Jumanne alizungumza kwa njia ya simu na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina na akasisitiza kuwa, anapinga mpango huo ulio kinyume na sheria wa utawala wa Kizayuni wa kuziunganisha baadhi ya sehemu za eneo la Ufukwe wa Magharibi na Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).  Mnamo tarehe 6 Julai pia Johnson alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na waziri mkuu mwenzake wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na akamtahadharisha na matokeo ya kulimega eneo la Ufukwe wa Magharibi, ambapo mbali na kueleza wasiwasi alionao juu ya kutekelezwa mpango huo, alibainisha kuwa, uamuzi huo unahatarisha matarajio ya kupatikana suluhu na amani katika eneo. Kabla ya hapo pia, waziri mkuu huyo wa Uingereza alitoa taarifa fupi akionya kuwa London haitayakubali mabadiliko yoyote ya mipaka iliyowekwa mwaka 1967 isipokuwa jamabo kama litafanyika hilo kwa ridhaa ya pande mbili. Mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina nchini Uingereza, siku ya Jumatano aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akitaka Israel iwekewe vikwazo; na wakati huohuo serikali ya Uingereza iitambue rasmi Palestina kama nchi huru. 

Msimamo huo ulioonyeshwa na London ambayo hivi sasa imejitoa kwenye Umoja wa Ulaya unaendana na msimamo wa umoja huo katika kupinga mpango wa kumegwa sehemu ya eneo la Ufukwe wa Magharibi na kuunganishwa na Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 11 za Ulaya wamemwandikia barua Mkuu wa Sera za Nje wa EU Josep Borell wakisema, wana wasiwasi kwamba muda wa kuratibu machaguo ya hatua ambazo itapasa zichukuliwe dhidi ya Israel endapo itatekeleza mpango wa kulimega eneo la Ufukwe wa Magharibi, unazidi kuyoyoma. Barua hiyo imeandikwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Italia, Uholanzi, Ireland, Ubelgiji, Luxemburg, Sweden, Denmark, Finland, Ureno na Malta kwa Mkuu wa Sera za Nje wa EU Josep Borell. Katika barua yao hiyo, mawaziri hao wa mambo ya nje wa nchi 11 wanachama wa Umoja wa Ulaya wametaka itayarishwe haraka orodha ya hatua ambazo umoja huo unaweza kuchukua dhidi ya utawala wa Kizayuni endapo utatekeleza mpango wa kumega asilimia 30 ya eneo la Ufukwe wa Magharibi na kuliunganisha na Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), na wakasisitiza kwamba, muda wa kuizuia Tel Aviv isitekeleze mpango huo unamalizika. 

Katika upande mwingine zaidi ya wabunge 100 kutoka vyama mbali mbali vya kisiasa Ufaransa wamemtaka Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo aitambue rasmi Dola la Palestina na kuongeza vikwazo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mpango wake wa kuteka ardhi za Ukingo wa Maghairbi.

3472024

captcha