IQNA

Ayatullah Ahmad Jannati

Kuwa na uhusiano na utawala bandia wa Israel hakutauzuia kusambaratika

12:10 - August 20, 2020
Habari ID: 3473086
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema kuwa, kuanzisha na kutangaza wazi kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel hakutauwezesha utawala huo ghasibu uendelee kubakia.

Ayatullah Ahmad Jannati amesema, hatua ya baadhi ya tawala zenye fikra mgando katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ya kutangaza wazi kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel hakuwezi kuusaidia utawala huo bandia na kuzuia usisambaratike.

Ayatullah Ahmad Jannati ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya hivi karibuni ya utawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel unaoua watoto na kusisitiza kwamba, hatua hiyo ya UAE ni kitendo cha kikhabithi na chenye doa chafu.

Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran  ameongeza kuwa, hata kama baadhi ya tawala za Ghuba ya Uajemi kama Saudi Arabia na Imarati kwa miaka mingi zimekuwa vna uhusiano wa siri na utawala wa Israel unaotenda jinai, lakini wananchi katika Ulimwengu wa Kiislamu katu hawawezi kusahau hiana na usaliti wa viongozi wao walioamua kujirahisisha kwa Israel.

Alhamisi iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza habari ya kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili. Hatua hiyo imeendelea kulaaniwa na watu huru na wapigania uadilifu kote ulimwenguni na hasa katika nchi za Kiislamu.

/3917591

captcha