IQNA

Waislamu Uingereza wataka China izuiwe kuwakandamiza Waislamu

22:34 - August 20, 2020
Habari ID: 3473088
TEHRAN (IQNA) – Waislamu nchini Uingereza wameitaka serikali ya nchi yao ichukue hatua kali dhidi ya China kutokana na kukandamizwa Waislamu wa jamii ya Uighur.

Katika taarifa, Baraza la Waislamu Uingereza (MCB), limesema ukandamizaji wa Waislamu wa jamii ya Uighur nchini China una sifa zote za jinai ya maangamizi ya umati. MCB imemuandikia barua Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ikimtaka achukue hatua dhidi ya China.

Barua hiyo imeashiria hali mbaya ya Waislamu katika eneo la Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, eneo ambalo ni makao ya Waislamu zaidi ya milioni 10 wa jamii ya Uighur.

Mwezi Julai pia, Mkuu wa Shirika la Kiislamu la Haki za Binadamu (IHRC) lenye makao yake London alilaani kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu ukandamizaji wa jamii za Waislamu waliowachache nchi mbali mbali duniani.

Akiashiria Kkuhusu Waislamu wa jamii ya Uighur nchini China, mwenyekiti wa IHRC Masoud Shajareh alisema wamekuwa wakiandamizwa na utawala wa China kwa muda mrefu sana. Amesema Waislamu wa jamii ya Uighur ni wapenda amani lakini wamekuwa wakibaguliwa na kukandamizwa.

Shajareh amesema IHRC imezindua kampeni kadhaa za kuwafahamisha walimwengu kuhusu Waislamu wanaokandamizwa duniani ikiwa ni pamoja na kukusanya misaada.

Kwa mujibu wa taarifa karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Uighur na jamii zingine za wanaozungumza Kituruki wanashikiliwa katika kambi maalumu za kuwapa mafunzo wa Kikomunisti kinyume cha matakwa yao  mkoani Xinjiang.

Hatahivyo,  mwezi Novemba mwaka jana China ilitoa taarifa na kupinga taarifa za kimataifa kuwa imewaweka Waislamu wa mkoa wa Xinjiang katika kambi maalumu kwa lengo la kuwabadilisha itikadi zao.

Kupitia taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilidai kuwa hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu au ukandamizaji wa kikabila na kidini katika mkoa wa Xinjiang na kwamba oparesheni za usalama katika mkoa huo zinalenga kukabiliana na ‘utumiaji mabavu na ugaidi’.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeongezeka sera za kuwakandamiza Waislamu katika nchi hiyo hasa katika jimbo la Xinjiang wenye Waislamu Zaidi ya milioni 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

3917848/

captcha