IQNA

Wananchi wa UAE wapinga uhusiano na utawala wa Israel

13:57 - August 23, 2020
Habari ID: 3473095
TEHRAN (IQNA) - Wanaharakati wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wameanzisha mkakati wa kupinga uhusiano wa nchi yao na utawala haramu wa Israel.

Wanaharakati hao wameyataja mapatano yaliyofikiwa kati ya nchi yao na utawala wa Kizayuni ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande mbili kuwa ni kukiuka katiba na na kupuuza msimamo wa viongozi wa mwanzo wa Imarati katika kuinga mkono Palestina.

Taarifa ya wanaharakati wa Imarati imeeleza kuwa, mapatano kati ya Abu dhabi na Tel Aviv yamepuuza  kifungu cha 12 cha katiba ya Imarati kinachosisitiza juu ya umoja huo wa Falme za Kiarabu kuunga mkono masuala yanayouhusu Umma na maslahi ya Kiarabu na Kiislamu na pia sheria nambari 15 ya mwaka 1972 inayohusu kuususia utawala wa Israel.  

Wanaharakati wa Imarati wameongeza kuwa, mapatano kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni ni sawa na kujitoa katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya uajemi, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) na hata katika maazimio ya Umoja wa Mataifa. 

Rais Donald Trump wa Marekani Agosti 13 mwaka huu alitangaza kufikiwa mapatano kati ya UAE na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuhuisha uhusiano kati ya pande mbili hizo.

/3918331

captcha