IQNA

Rais Hassan Rouhani

Utamaduni wa Ashura umeiwezesha Iran kuwashinda maadui

22:13 - August 26, 2020
Habari ID: 3473107
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia siku hizi za maombolezo na kukumbuka mauaji ya Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW na kusema: "Taifa la Iran limepata ushindi kwa kusimama kidete na kupambana na njama za madola makubwa, na ushindi huo umetokana na kufuata utamaduni wa Ashura."

Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa, vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa dhidi ya Iran mwaka 2018 vimesababisha upungufu wa takribani dola bilioni 50 katika pato la nchi na kuongeza kuwa: "Mahesabu ya adui yalikuwa sahihi katika hali ya kawaida, lakini kutokana na kuwa wananchi wa Iran walitegemea utamaduni wa Ashura katika kusimama kidete na kupambana na adui, adui ameshindwa licha njama za kila uchao."

Imam Hussein AS, Imamu wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani aliuawa shahidi mwaka 61 Hijria katika ardhi ya Karbala katika siku ya 10 ya mwezi wa Muharram, siku ambayo ni maarufu kama Ashura. Imam Hussein AS alijitolea mhanga na kufa shahidi katika jangwa la Karbala na harakati yake hiyo imebakia kuwa somo la daima la kupigania uhuru na kujiheshimu kwa wanadamu wote.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameashiria njama za maadui kwa ajili ya kulipigisha magoti taifa la Iran na kusema:" Kwa kusimama kidete na muqawama mbele ya njama na mashinikizo, taifa la Iran limemzuia adui kutimiza malengo yake ya kusambaratisha mfumo wa Kiislamu."

Rouhani amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, taifa la Iran limekabiliwa na mashinikizo makali zaidi lakini pamoja na hayo miradi muhimu ya maendeleo imezinduliwa katika kipindi hicho. Ameongeza kuwa, katika hali ambayo baada ya janga la corona watu wa nchi za Magharibi waliingiwa na wahka mkubwa kutokana na ukosefu wa bidhaa muhimu za kila siku lakini wananchi wa Iran hawajakumbwa na ukosefu wa bidhaa muhimu ambazo zote zinazalishwa ndani ya nchi.

3919161

captcha