IQNA

Iran yalaani hatua ya jarida la Ufaransa kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

21:36 - September 04, 2020
Habari ID: 3473135
TEHRAN (IQNA) - Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali hatua ya jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo ya kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW).

Saeed Khatibzadeh amesema kitendo chochote cha kumdhalilisha na kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad (saw) au Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu ni jambo lisilokubalika kabisa.

Amebainisha kuwa: Hatua hiyo ya kichochezi kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, kimeumiza hisia za wafuasi wa dini zinazomuabudu Mungu Mmoja kote duniani, mbali na kuvunjia heshima thamani, mafundisho na imani ya Waislamu zaidi ya bilioni moja duniani kote.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kinyume kabisa na kitendo hicho cha kichokozi cha jarida hilo la Ufaransa, lakini uhuru wa kujieleza ni kitu chenye thamani kubwa ambacho kinapaswa kutumiwa kujenga umoja, utangamano na kuishi kwa amani jamii yote ya wanadamu, pasi na kujali tofauti zao za kidini.

Kwa mara nyingine tena jarida hilo la Kifaransa la Charlie Hebdo limeamua kwa makusudi kuwafanyia kejeli na istihzai Waislamu na dini tukufu ya Uislamu kwa kuchapisha vibonzo hivyo Jumatano ya juzi, siku ya kuanza kwa kesi dhidi ya watuhumiwa wa shambulizi dhidi ya ofisi ya jarida hilo mnamo Januari 7 mwaka 2015.

Chokochoko hizo za Charlie Hebdo ya Ufaransa zimezusha wimbi kubwa la ghadhabu, maandamano na malalamiko katika maeneo mbalimbali duniani.

3472457

captcha