IQNA

Kiongozi wa Hamas ataka Wapalestina waungane kukabiliana na njama za Marekani na Israel

21:42 - September 04, 2020
Habari ID: 3473136
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniya kwa mara nyingine tena amesisitiza udharura wa kuungana na kushirikiana makundi yote ya kisiasa na kijamii ya Palestina kwa lengo kuzima njama za maadui zao, yaani utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na baadhi ya tawala za kizandiki za Kiarabu.

Haniya aliyasema hayo jana Alkhamisi akiwa katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut alikoenda kushiriki kikao cha makundi ya muqawama ya Palestina, sambamba na kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa Lebanon, akiwemo Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.

Ameeleza bayana kuwa, "tumekutana hii leo kutangaza kuwa Wapalestina watasimama pamoja ama ndani ndani au nje ya Palestina. Hivi sasa tunapitia kipindi hatari na nyeti mno ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Kipindi hiki kimebeba tishio la kistratajia kwa kadhia ya Palestina na kwa kanda nzima kwa jumla."

Sambamba na kusisitiza kuwa utawala haramu wa Israel unasalia kuwa adui nambari moja wa Wapalestina, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya HAMAS amesema hatua ya baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu ya kufanya wa kawaida uhusiano wao na Israel, haitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kupotosha zaidi historia na jiografia ya eneo la Asia Magharibi.

Ziyad al-Nakhalah, kiongozi wa harakati ya Jihadul Islami ambayo makao yake yako katika Ukanda wa Gaza kama ya HAMAS, ni miongoni mwa shakhsia wa Palestina walioshiriki mkutano huo wa jana mjini Beirut. Aidha Mahmoud Abbas, rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameshiriki mkutano huo kwa njia ya video akiwa mji wa Ramallah, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, eneo linalilokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.

Haniya ameutaja 'Muamala wa Karne' unaoshinikizwa na Marekani kama kibali 'kisicho cha kawaida' cha Washington kwa Tel Aviv cha kuendelea kukanyaga haki za msingi za Wapalestina.

3472455

captcha